(IQNA) – Darsa za Qur’ani za majira ya kiangazi, zilizoandaliwa kwa ajili ya mabinti na Taasisi ya Qur’ani Tukufu katika Ataba (Idara ya Usimamizi wa Haram) Tukufu ya Imam Hussein (AS) mjini Karbala, Iraq, Imefikia tamati yake.
Kuhitimishwa kwa madarasa haya kuliadhimishwa kwa hafla maalum iliyofanyika katika Sahn Tukufu, kuashiria kilele cha kipindi cha mafunzo kilichojaa shughuli za kielimu na malezi ya kiroho.
Bi. Amal Al-Mutawari, afisa anayesimamia shughuli za Qur’ani, aliliambia shirika la habari la Karbala Now kuwa sherehe za kuhitimisha zimeakisi juhudi kubwa zilizofanywa katika kipindi chote cha mafunzo. Tukio hilo liliungwa mkono na idara mbalimbali za Ataba tukufu, zikiwemo Idara ya Usalama, Idara ya Ukarabati na Matengenezo, Idara ya Usafirishaji, pamoja na Kitengo cha Zaynabiyat na wafanyakazi wa Taasisi ya Qur’ani.
Alieleza kuwa darsa hizo zilifanyika kwa siku kadhaa, kuanzia saa mbili asubuhi (8:00 a.m.) hadi saa tano asubuhi (11:00 a.m.), yakilenga zaidi mafunzo ya hifdhi na tilawa ya Qur’ani. Kwa mujibu wa Bi. Mutawari, mabinti katika ngazi ya kati na maandalizi walihifdhi sehemu ya Qur’ani inayolingana na urefu wa Surah Al-Baqarah, huku wanafunzi wa shule za msingi wakizingatia hifdhi ya Juzuu ya 29.
Mafunzo hayo hayakuishia kwenye elimu ya Qur’ani pekee, bali yalihusisha masomo ya Fiqh ya Kiislamu, Akhlaq, na malezi ya maadili. Shughuli hizi ziliandaliwa kwa lengo la kujenga haiba bora na kuimarisha uhusiano wa mabinti hawa na Qur’ani Tukufu pamoja na mafundisho mema ya Ahlul-Bayt (AS).
Bi. Mutawari aliongeza kuwa Taasisi ya Qur’ani ina mpango wa kudumisha mawasiliano na washiriki hata baada ya madarasa hayo kumalizika, kwa kuanzisha chaneli maalum ya Telegram. Chaneli hiyo itarahisisha ushirikiano endelevu na kuratibu programu mbalimbali za Qur’ani kwa mwaka mzima, ikiwa ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuendeleza elimu ya dini.
3498938
Zenye maoni mengi zaidi