(IQNA) – “Kongamano la Kimataifa la Miujiza ya Kisayansi Katika Qur’ani na Sunnah” limezinduliwa rasmi siku ya Jumatatu katika mji mtakatifu wa Makkah al-Mukarramah.
Dkt. Mohammed Al-Issa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu (MWL-Rabita) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, ndiye aliyeongoza hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo la kitaaluma.
Shughuli hiyo ilianza katika makao makuu ya Jumuiya hiyo mjini Makkah, ikihudhuriwa na kundi teule la wanazuoni bingwa na wataalamu kutoka kila pembe ya ulimwengu wa Kiislamu.
Katika sehemu ya kongamano hilo, pia kulizinduliwa Ensaiklopidia ya Rabita ya Miujiza ya Kisayansi Katika Qur’ani na Sunnah.
Hii ni ensaiklopidia ya kwanza ya kidijitali na ya kiutangamano ya aina yake katika uwanja huu, ikiwa inapatikana katika lugha kumi tofauti.
Ensaiklopidia hiyo inajumuisha makala 500 za utafiti wa kisayansi zilizohakikiwa na wataalamu, zikijumuisha kurasa 7,500 zilizogawanywa katika majalada 15. Kazi hii inaambatana na picha 2,000 za kisayansi zenye ubora wa hali ya juu, video 2,000 fupi za kisayansi, pamoja na viunganishi 4,000 vinavyoelekeza kwenye tovuti za kisayansi zinazoaminika na majarida ya kitaaluma yaliyohakikiwa.
Katika hitimisho la uzinduzi huo, wanazuoni kadhaa waliotoa michango mikubwa ya kiutafiti na kitaaluma katika fani ya miujiza ya kisayansi walitunukiwa heshima maalum kwa juhudi zao tukufu.
3498940
Zenye maoni mengi zaidi