(IQNA) – Waziri wa Mambo ya Kiislamu wa Maldives (Maldivi), Dkt. Mohamed Shaheem Ali Saeed, amesema kuwa zaidi ya wanafunzi 2,000 kwa sasa wanajifunza kuhifadhi Qur’ani Tukufu nchini humo.
Waziri alitamka kuwa ongezeko la idadi ya wahifadhi Qur'ani nchini Maldives ni jambo la kufurahisha na la faraja. Hasa, anawaona vijana wanaohifadhi Qur’ani Tukufu kuwa ni mwanga unaoongaza mustaqbali wa Kiislamu wa taifa hilo la Kisiwa.
“Hadi sasa, idadi ya Wahifadhi (Huffaadh) nchini Maldives imefika 322. Ramadhani ijayo, Insha-Allah, inatarajiwa kuwa idadi kubwa ya Wahifadhi watahitimu,” alisema waziri huyo.
Dkt. Shaheem alitangaza kuwa serikali inaipa kipaumbele kikubwa kuongeza idadi ya Wahifadhi, huku lengo likiwa ni kuinua idadi hiyo hadi 500 katika muhula huu wa uongozi. Waziri pia alibainisha kuwa Rais Dkt. Mohamed Muizzu ameongeza mshahara wa serikali unaotolewa kwa Wahifadhi ili kuwahamasisha.
Waziri pia aliyeleza kuwa miradi ya uhifadhi wa Qur’ani Tukufu imepanuliwa.
Alitamka kuwa hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 2,000 katika Visiwa vyote vya Maldives wanajifunza kuhifadhi Qur’ani Tukufu, huku idadi kubwa ya wanafunzi wakisoma katika Kituo cha Qur’ani Tukufu na Taasisi ya Ilm.
Chini ya sera iliyowekwa na serikali ya kupanua elimu ya Qur’ani kote katika visiwa vyote vya Maldives, matawi ya Kituo cha Qur’ani Tukufu yamesajiliwa na kuanza kufanya kazi kwa ufanisi katika visiwa 30. Waziri aliongeza kuwa jitihada zinaendelea kusajili maeneo mengine 20.
“Kazi inaendelea kujenga maeneo mengine 38. Lengo ni kufikisha mradi huu katika visiwa vyote ndani ya miaka miwili ijayo,” alisema waziri huyo.
Waziri alitangaza kuwa katika matawi ya Kituo cha Qur’ani yaliyopo visiwani, wajibu wa kufundisha Qur’ani Tukufu pia unaongezwa kwenye majukumu rasmi ya Waimamu.
3498949
Zenye maoni mengi zaidi