(IQNA) – Kampuni ya zana za michezo ya Adidas imetoa msamaha rasmi kufuatia malalamiko makubwa na ukosoaji mkali dhidi ya kampeni yake ya kikanda iliyomshirikisha mwanajeshi wa zamani wa Israel. Hatua hiyo imelaaniwa vikali na Wapalestina waliokatwa viungo katika vita vya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, wakati wakipambana kupata viungo bandia vya msingi na huduma za ukarabati wa kimatibabu.
Mzozo huo unatokana na kuonekana kwa Shalev Biton, mwanajeshi wa zamani wa Israel aliyepoteza mguu wake, katika kampeni ya ndani ya kutangaza huduma ya Adidas ya “Single Shoe” (Kiatu Kimoja) — mradi maalum uliotengenezwa kwa ajili ya watu waliokatwa miguu au wale wanaohitaji kiatu kimoja tu. Picha za kampeni hiyo zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo watumiaji wanaounga mkono Palestina walilinganisha fursa aliyonayo Biton ya kupata viungo bandia vya kisasa na hali mbaya inayowakabili maelfu ya waathirika wa jinai za Israel huko Gaza.
Kwa Wapalestina waliopo katika ukanda huo uliozingirwa na Israel, kampeni hiyo imedhihirisha ulimwengu wenye sura mbili tofauti kabisa.
“Inakuwaje Adidas inamleta mwanajeshi wa Israel na kumweka kwenye tangazo wakati sisi, majeruhi wa vita hapa Gaza, tunateseka kiasi hiki?” aliuliza Omar Haliwa, kijana mwenye umri wa miaka 14 aliyepoteza mguu wake katika shambulio la Israel alipokuwa njiani kwenda kuchota maji. Alieleza kuwa juhudi zake za kupata kiungo bandia kinachofaa zimekwama mara kwa mara kutokana mechemko na uhaba mkubwa wa malighafi katika vituo vya viungo bandia mjini Gaza.
Kifah al-Fakhouri, aliyepoteza mguu wake kufuatia shambulio la Israel lililolenga mkahawa wa pwani jijini Gaza, alisema alisikitishwa na kushtushwa sana na kampeni hiyo. “Mwanajeshi huyu alipoteza mguu wake mwaka 2021 na sasa ana kiungo bandia pamoja na rasilimali zote. Sisi hapa Gaza hatuna chochote, hatuna matibabu, hatuna vifaa, wala fursa yoyote,” aliwaambia waandishi wa habari wa Shirika la Anadolu.
Ahmed Jawadi al-Balawi, Mpalestina mwingine aliyekatwa mguu, alitoa ombi la moja kwa moja kwa kampuni hiyo: “Tuanangalieni kwa huruma. Wao hawahitaji msaada kama sisi. Wana rasilimali zote; sisi hatuna chochote.”
Kwa mujibu wa Dkt. Munir al-Barsh, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Gaza, makadirio yanaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 8,000 wamepoteza viungo vyao wakati wa vita vya Israel dhidi ya Gaza, ikijumuisha zaidi ya watoto 3,000. Alibainisha kuwa Gaza inao wataalamu waliosomea utengenezaji wa viungo bandia, lakini vikwazo vya Israel katika uingizaji wa malighafi na vifaa vya kimatibabu vimezuia wagonjwa wengi kupata huduma zinazofaa.
Kufuatia malalmiko hayo ya ukosoaji na wito wa kususia bidhaa za Adidas uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akaunti ya kikanda ya Mashariki ya Kati, Adidas Arabia, ilitoa taarifa ya msamaha ikisema kuwa picha iliyotumika katika tangazo hilo la ndani imeibua “wasiwasi na hisia kali.”
“Haikuwa nia yetu kukwaza au kuumiza hisia za mtu yeyote, na tunaomba msamaha kwa wote walioathirika,” ilisema taarifa hiyo, ikisisitiza kuwa tangazo hilo lilikuwa mpango wa kikanda na wala si sehemu ya kampeni ya kimataifa. Adidas Arabia pia iliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea “kusikiliza, kujifunza na kufanya kazi” ili kuhakikisha kuwa hatua zake zinaakisi maadili yake ya usawa na ujumuishaji.
Hata hivyo, kwa waathirika waliokatwa viungo huko Gaza, mzozo huo umeonyesha pengo kubwa linalozidi mipaka ya tangazo moja la biashara. Kampeni moja ilimweka mlemavu mmoja katika mwangaza wa umaarufu, huku maelfu ya wengine huko Gaza bado wakisubiri fursa ya kuweza kutembea tena.
3498948
Zenye maoni mengi zaidi