IQNA

11:50 - September 09, 2026
Habari ID: 3482743

Mahafidh 300 wa Qur’ani waenziwa huko Gaza

IQNA — Taasisi ya Wakfu ya Hedai ya Uturuki imewatunuku heshima zaidi ya wanafunzi 300 wa kiume na wa kike katika Ukanda wa Gaza ambao wamefanikiwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Wanafunzi hao walitunukiwa katika hafla iliyofanyika mjini Deir al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza, mwishoni mwa juma lililopita, licha ya hali ngumu na ya kuhuzunisha wanayopitia wakaazi wa eneo hilo kutokana na vita vya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Uwanja wa michezo wa Annan, ulioko karibu na lango la kuingilia Deir al-Balah, ndio uliokuwa mwenyeji wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na familia za wanafunzi, wanazuoni wa Kiislamu, pamoja na shakhsia mashuhuri. Shughuli hiyo ilijumuisha upigaji wa wimbo wa taifa wa Palestina, kaswida na maombi (dua), kisha kufuatiwa na kuwavika taji na kuwatunuku mahafidh hao wa Qur’ani.

Bilal Abutayr, mwakilishi wa Taasisi ya Hedai, aliliambia Shirika la Habari la Anadolu kwamba hafla hii inaakisi juhudi za mtandao wa shule za taasisi hiyo katika Ukanda wa Gaza, unaohudumia zaidi ya wanafunzi 10,000 kupitia miradi yake ya kielimu na misaada ya kibinadamu.

Aliongeza kuwa wanafunzi hao mahiri walivumilia mazingira magumu mno wakati wa vita vya maangamizi ya umati vya Israel; baadhi yao walipoteza makazi na jamaa zao, huku wengine wakiwa ndio manusura pekee waliosalia katika familia zao.

Abutayr alibainisha kuwa mahafidh hao walistahimili hasara na changamoto nzito kama vile kukatika kwa umeme mara kwa mara, joto kali ndani ya mahema, njaa, na uhaba wa maji safi, lakini waliendelea na juhudi zao za kuhifadhi Qur’ani ili kufikisha ujumbe mzito kwamba ardhi hii ina tunu yenye kustahili kuishi kwayo, na kwamba watu wa Palestina ni jamii yenye uhai, msimamo imara, na inayoshikamana na miongozo ya Qur’ani Tukufu.

Shazi Hamad, mmoja wa mahafidh waliotunukiwa heshima hiyo, alisema kuwa kutokana na wimbi la kufurushwa makazini, mashambulizi ya mabomu, na uharibifu mkubwa ulioshuhudiwa Gaza, kazi ya kuhifadhi Qur’ani haikuwa rahisi hata kidogo.

Alieleza kuwa licha ya mashambulizi na kuhama makazi mara kwa mara, “Nilikuwa na azma na msimamo thabiti wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu, na alhamdulillah, niliihifadhi yote kwa fadhila na baraka za Mwenyezi Mungu, pamoja na usaidizi na dua za wazazi na dada zangu.”

3498956

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu gaza
captcha