IQNA— Polisi wameanzisha uchunguzi baada ya kanda ya video kusambaa ikimuonyesha mwanamume akitupa vipande vya nyama ya nguruwe katika Msikiti wa Warragul ulioko Gippsland, jimbo la Victoria, Australia, mnamo mchana wa Jumatano. Kitendo hiki cha chuki kimeiacha jamii ya Kiislamu ya eneo hilo ikiwa na huzuni na majonzi.
Picha za kamera za usalama zinamwonyesha mwanamume aliyevaa nguo za michezo za kijivu akitupa nyama hiyo karibu na mlango wa msikiti huo. Tukio hili, ambalo viongozi wa kijamii wamelitaja kuwa la chuki na dharau, lilitokea siku chache baada ya mtu maarufu kwenye mitandao ya kijamii, anayejinasibu kama mtetezi wa “Ukristo” nchini Australia, kuposti video ya msikiti huo ambao ulifunguliwa mwaka jana.
“Njia kuu ya kujilinda dhidi ya ushindi wowote ni kuufanya Ukristo wetu uwe na nguvu tena,” ujumbe wa Nick Patterson ulisomeka. “Fisi watashambulia kila wanapohisi kuna udhaifu. Tunahitaji kuwa simba tena.”
Bidhaa za nguruwe hutumiwa mara kwa mara katika mashambulizi ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kwa sababu ulaji wa nguruwe ni haramu katika Uislamu. Vipande vya nyama hiyo vilionekana vimetapakaa kwenye ngazi za msikiti. Uongozi wa Msikiti wa Warragul umetaja shambulio hilo kuwa jaribio la “kukwaza, kutisha, na kugawanya jamii.”
“Jaribio hilo halitafanikiwa,” msikiti huo ulisema katika taarifa yake.
Msikiti huo ulifunguliwa mwaka jana katika jengo ambalo hapo awali lilikuwa kanisa, baada ya Kanisa la Uniting kuhamia eneo jipya miaka ishirini iliyopita. Msikiti huo ulianzishwa kama nafasi wazi na shirikishi inayotoa mahali pa sala na mikusanyiko kwa jamii inayokua ya Waislamu katika eneo hilo.
Mansoor Shamsi, makamu mwenyekiti wa Kamati ya Msikiti wa Warragul, alisema msikiti huo umewahi kulengwa kwa maandishi ya chuki na uharibifu hapo awali. “Kwa bahati mbaya, [sijashangazwa] wala sijashtushwa,” alisema. “Tupo katika hali ya kutotaka kupa nafasi jambo ambalo halistahili tahadhari yoyote kwa sababu linatoka katika ujinga, chuki, na hofu. Wakati huo huo, tunahisi tuna wajibu wa kukemea vitendo hivyo.”
Polisi wa Victoria wamesema wanaendelea kuchunguza tukio hilo. Rais wa Baraza la Kiislamu la Victoria (ICV), Mohamed Mohideen, alisema suala hilo ni lenye kuumiza kwa jamii pana ya Waislamu na linaonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu.
“Hatupo hapa kuteka makanisa,” alisema. “Hatupo hapa kuteka imani ya watu au kudhoofisha imani ya wengine.”
Mnamo mwezi Julai, ICV iliwasilisha ripoti kwa polisi baada ya makaburi ya Waislamu katika Makaburi ya Maddingley kulengwa kwa vibandiko vyenye picha za nguruwe. Mohideen alisema matukio kama haya yanajaribu — na kushindwa — kuchochea hisia kutoka kwa jamii ya Waislamu. “Jamii ni imara sana,” alisema. “Waislamu wamezoea mashambulizi ya chuki dhidi ya Uislamu.”
Mansoor Shamsi aliongeza kuwa Msikiti wa Warragul umepokea “ungwaji mkono mkubwa” kutoka kwa jamii pana. Kiongozi wa chama cha Greens katika jimbo la Victoria, Ellen Sandell, alikemea tukio hilo, akiliita “kitendo cha kinyama na cha makusudi cha chuki ya Uislamu.”
“Kila kiongozi wa kisiasa ana wajibu wa kufanya kila awezalo ili kukemea kwa sauti ongezeko la mashambulizi haya ya kinyama na ya kibagazi, na kupambana dhidi ya itikadi kali za mrengo wa kulia zinazochochea vitendo hivi,” Sandell alisema. “Chama cha Greens kinasimama bila kuyumbayumba na Msikiti wa Warragul pamoja na jamii za Kiislamu kote Victoria. Hapatakuwa na nafasi ya uvumilivu kwa chuki dhidi ya Uislamu, au aina yoyote ya ubaguzi wa rangi huko Victoria.”
Siku mbili kabla ya tukio la Septemba 9 msikitini hapo, aliyekuwa mpiganaji wa ndondi za mchanganyiko (MMA), Nick Patterson, aliposti video ya Msikiti wa Warragul kwenye ukurasa wake wa Facebook. Katika siku zilizofuata, posti yake ilivutia mamia ya maoni kutoka kwa watu waliokasirishwa na ukweli kwamba msikiti huo unatumia jengo la zamani la kanisa, licha ya ukweli kwamba kanisa hilo liliacha ibada hapo tangu mwaka 2006. Baadhi ya maoni yalipendekeza kuwa eneo hilo linapaswa kuharibiwa kwa bidhaa za nguruwe.
Polisi wa Victoria wametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu tukio hilo kuwasiliana na idara ya Crime Stoppers.
3498983
Zenye maoni mengi zaidi