IQNA — Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka na mipaka ya Yemen.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inathibitisha tena msimamo wake wa kimsingi na usioyumba kuhusiana na haja ya kuheshimu mamlaka ya kitaifa na uadilifu wa mipaka ya Yemen, pamoja na umuhimu wa kukomesha mzingiro wa kinyume cha sheria na usio na utu dhidi ya nchi hiyo,” ilisema wizara hiyo katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi.
“Bila shaka, usalama na utulivu katika Asia Magharibi na ukanda wa Bahari ya Sham haviwezi kupatikana bila kulinda haki halali na utu wa watu wakuu wa Yemen.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa matukio ya sasa nchini Yemen hayawezi kutazamwa kwa kutengwa na maendeleo yaliyotokea katika muongo uliopita.
“Watu watukufu wa Yemen ambao ni warithi wa ustaarabu wenye kung’aa na wa kihistoria ambao siku zote wamecheza nafasi muhimu na ya fahari katika historia ya kikanda na kimataifa, wana haki ya kuishi maisha ya heshima bila shinikizo, vitisho, na mzingiro wa kukandamiza, na kuwa na mamlaka yao ya kitaifa na uadilifu wa mipaka kuheshimiwa kikamilifu.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza haja ya kuzingatia maslahi ya Umma wa Kiislamu, hasa katika wakati huu ambapo eneo la Asia Magharibi linakabiliwa na uovu, ukandamizaji, na upanuzi wa kipekee wa utawala wa Kizayuni, unaosaidiwa na Marekani, na kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza tena kuwa kutatua masuala yanayohusiana na Yemen hakuwezekani kupitia mizingiro inayoendelea au ushirikiano wa kijeshi.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza haja ya kuanzishwa mara moja kwa mazungumzo kulingana na ramani ya barabara iliyokubaliwa na utekelezaji wa masharti yake, na iko tayari kutoa huduma zake njema kuwezesha mchakato huu,” taarifa hiyo ilihitimisha.
Taarifa hiyo imekuja huku Jeshi la Yemen lilifanikiwa kudhibiti kikamilifu Lango-Bahari muhimu mno la Bab al-Mandab baada ya kukikomboa kisiwa cha kimkakati cha Mayun. Hilo ni pigo kubwa kwa wavamizi wote wa Yemen.
Kukombolewa kisiwa cha kimkakati cha Mayun , ambacho kinajulikana kama eneo muhimu la kimkakati katikati ya Lango-Bahari la Bab al-Mandab , kumesababisha njia hiyo muhimu ya majini kuwa chini ya udhibiti kamili wa serikali ya Sana'a.
Jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuchukua udhibiti wa Kisiwa cha Mayun na hivyo kuimarisha zaidi udhibiti wake wa Lango-Bahari la Bab al-Mandab ambalo ni muhimu mno kwa safari za vyombo vya baharini duniani.
Hatua hiyo imefuatia kutekwa hivi karibuni mji wa bandari wa Mocha (Al-Mukha) na jeshi la Yemen, jambo lililolazimisha askari vibaraka wa Saudia Arabia kukimbia na kuelekea kusini, katika mji wa Dhubab.
/3498982
Zenye maoni mengi zaidi