IQNA— Washindi wa toleo la kwanza la kitengo maalum cha kimataifa cha mayatima kiitwacho “Rofaqa,” ambacho ni sehemu ya Mashindano ya Qur’ani Tukufu ya Sheikh Jassim bin Mohammed bin Thani, wametiwa moyo na kuenziwa katika hafla maalum iliyofanyika nchini Qatar.
Wizara ya Wakfu na Mambo ya Kiislamu ya nchi hiyo, kwa ushirikiano na shirika la Qatar Charity, ndiyo iliyowaenzi washindi wa mashindano hayo.
Toleo hili la kwanza lilipata muitikio mkubwa duniani, likiwashirikisha washiriki yatima 389 wanaofadhiliwa, wenye umri wa miaka 12 hadi 20. Kati yao, washiriki 278 kutoka nchi 20 walipenya hadi hatua za awali, hatimaye kufika kwa washindi 30 wa fainali kutoka nchi nane waliochuana jijini Doha katika kategoria tatu kuu.
Katika hafla hiyo ya utoaji tuzo, Mkuu wa Kamati ya Maandalizi, Jassim Abdullah Al Ali, alibainisha kuwa mpango wa “Rofaqa” unaunganisha kwa kipekee huduma ya Qur’ani na utoaji wa misaada ya kibinadamu, jambo linalosaidia kulea tabia njema za mayatima hao na kuimarisha vipaji vyao vya Qur’ani.
Tuzo na heshima za juu zilitolewa katika kategoria tatu, ikianza na kitengo cha kuhifadhi Qur’ani nzima ambapo Abdulgani Abdulqadir Sheikh alishika nafasi ya kwanza na kujinyakulia kitita cha QAR 15,000. Alifuatiwa na wenzake, Abdulrahman Qasim Mohammed (nafasi ya pili, QAR 12,000) na Abdulrahman Ahmed Mahmoud (nafasi ya tatu, QAR 10,000). Wote hawa ni raia wa Somalia.
Katika kategoria ya kuhifadhi juzuu 20, Mohammed Qamaruzzaman kutoka Bangladesh alishika nafasi ya kwanza (QAR 10,000), akifuatiwa na Humam Mamoun Ziadeh kutoka Syria (nafasi ya pili, QAR 8,000), na Mohamadi Gumtebo Nana kutoka Burkina Faso (nafasi ya tatu, QAR 7,000).
Katika kategoria ya kuhifadhi juzuu 10, Mohammed Tafsir Amad Jalo kutoka Gambia alishika nafasi ya kwanza (QAR 7,000), akifuatiwa na Najm Al-Thaqib Chowdhury (nafasi ya pili, QAR 5,000) na Rehad Islam Mohammed Zahir (nafasi ya tatu, QAR 3,000), wote wakiwakilisha Bangladesh.
Mpango huu unakwenda sambamba na malengo ya kimkakati ya Wizara ya Wakfu ya Qatar, ambayo inalenga kuimarisha maadili ya Kiislamu na kuleta athari endelevu na zenye manufaa ndani ya jamii.
3498979
Zenye maoni mengi zaidi