IQNA – Historia ya usomaji wa Qur’ani Tukufu (Qiraa) katika Ulimwengu wa Kiislamu, na hususan nchini Misri, inavuka mbali zaidi ya zama za kuanza kurekodi sauti na matangazo ya redio.
Hii ni sanaa yenye mizizi mirefu iliyoanzia karne za kwanza za Uislamu; ikitegemea qiraa yenye mahadhi na lahni za kuvutia, sanaa hii iligeuka hatua kwa hatua kuwa moja ya nguzo zenye nguvu zaidi za ushawishi wa kiutamaduni wa Waislamu. Ilipata ukomavu wake wa kisanaa na kijamii kupitia nyanja kama vile qiraa za Swala ya Ijumaa, adhana, shughuli na ibada za kidini, pamoja na udhamini wa serikali na wafalme.
Ingawa Misri ndiyo chimbuko kuu la fani ya qiraa katika Ulimwengu wa Kiislamu, katika mazingira ya kisasa ya vyombo vya habari tunashuhudia “kusahaulika polepole kwa shule za asili za qiraa (madaris al-asliyyah)” na “kukatika kwa mawasiliano kati ya kizazi kipya cha wasomaji (qurraa’) na urithi wa watangulizi wao.”
Hivi sasa, baadhi ya visomo vya kibiashara na vya kijuujuu vimechukua nafasi ya qiraa zenye thamani ya kisanaa na zinazoamsha tafakuri. Aidha, kanuni na mbinu thabiti za Waqf (kusimama), Ibtida (kuanza), Maqamat (toni/sauti) na Tajweed, ambazo ni matunda ya uzoefu wa karne nyingi wa magwiji wa Misri, hazijaandikwa wala kutangazwa ipasavyo kwa kizazi cha sasa.
Kupitia mfululizo huu wa makala, IQNA inakusudia kufuatilia chimbuko na mageuzi ya sanaa hii, kuanzia “shule ya kale” hadi kuibuka kwa “magwiji na miamba ya qiraa”, huku ikitathmini hali ya sasa ili kujenga daraja kati ya mbinu asilia za Kimisri na mahitaji ya kisanaa ya wasikilizaji wa Qur’ani wa leo; lengo likiwa ni kuirejesha sanaa ya qiraa kutoka kwenye “ada ya kuiga tu” na kuifanya iwe “harakati hai na yenye nguvu.”
Licha ya kuwa teknolojia ya kurekodi sauti iliingia nchini Misri mnamo mwaka 1903, sanaa ya qiraa ya Qur’ani haikufaidika mara moja na maendeleo hayo ya kisasa kwa miongo kadhaa. Katika miaka ya awali ya makampuni ya kurekodi nchini Misri, wasomaji nguli walikataa kurekodi sauti zao. Kusita huku kulikuwepo pia miongoni mwa waimbaji, ambao walikuwa na wasiwasi na uvumbuzi huo mpya na walipendelea kusubiri, wakitazama kwanza mafanikio yake kupitia waimbaji wa daraja la pili, kabla ya wao wenyewe kujitosa.
Hali ilikuwa ngumu zaidi kuhusiana na Qur’ani Tukufu; kila ulipojitokeza uvumbuzi mpya uliogusa Qur’ani, ulikabiliwa na shaka pamoja na vikwazo vya kidini (tahadhari za kifiqhi). Kukubalika kwake mara nyingi kulicheleweshwa hadi kupita kwa muda kukaudhibitisha uvumbuzi huo, na kuufanya ukubalike kama sehemu ya kawaida ya zama husika.
Zaidi ya hayo, ufupi wa muda wa kurekodi katika miaka hiyo ya mwanzo, awali ukiwa dakika tatu tu, na baadaye kuongezwa hadi dakika sita, huenda ulichangia ucheleweshaji huo. Bila shaka, muda mfupi kama huo haukutosha kunasa qiraa kamili iliyoakisi uzito na thamani halisi ya sanaa hiyo kama ilivyokuwa ikitekelezwa wakati huo.
Qiraa ya Kwanza Kabisa Kurekodiwa Nchini Misri
Kipande cha zamani zaidi cha qiraa ya Qur’ani kilichosalia kinarejea mwaka 1905, kikiwa na sauti ya Sheikh Muhammad Salim akisoma Surah Maryam. Mwaka uliofuata, alirekodi qiraa nyingine, safari hii ikitoka Surah Yusuf.
Mengi hayajulikani kuhusu msomaji huyu, ingawa pia yapo marekodi ya nyimbo zake, jambo linaloacha sintofahamu iwapo alikuwa msomaji mahiri na mashuhuri wa Qur’ani au alikuwa mwimbaji wa kawaida tu aliyerekodi aya hizo kama sehemu ya majaribio ya awali ya makampuni ya kurekodi sauti.
Utafiti juu ya historia ya wasomaji wakubwa katika robo ya kwanza ya karne ya 20 unatuongoza kwenye majina manne maarufu ambayo sauti zao zimepotea katika kurasa za historia: Mahmoud Al-Qaisuni, Hussein Al-Sawwaf, Hanafi Bar’i, na Sheikh Ahmed Nada, huyu wa mwisho akiwa gwiji wa sanaa hii aliyeaga dunia mwaka 1932, miaka miwili kabla ya kuanzishwa kwa Idhaa ya Redio.
Kuzinduliwa kwa redio kulikuwa tukio la kihistoria na la mabadiliko makubwa lililonasa kumbukumbu za awali zilizorekodiwa za wasomaji mahiri kama Sheikh Muhammad Rif’at (1882–1950). Alizindua Idhaa ya Misri kwa sauti yake adhimu mnamo Mei 31, 1934, akijipatia nafasi ya kudumu katika historia kama mmoja wa waasisi wakuu wa sanaa hii ya usomaji.
Ingawa Sheikh Rif’at alikuwa tayari anajulikana miongo kadhaa kabla ya kuanzishwa kwa redio kutokana na sauti yake ya kipekee, yenye mvuto na hisia nzito za kiroho, chombo hicho cha habari kilimpa sifa ya kutokusahaulika milele. Kwa takriban muongo mzima, alibaki kuwa qari maarufu zaidi kwa hadhi na kupendwa, nyota wa redio aliyelinganishwa tu na nguli wa muziki kama Umm Kulthum na Abdel Wahab, hadi maradhi yalipomzuia kuendelea kusoma mwaka 1943. Alibaki na nafasi ya pekee ndani ya nyoyo za wasikilizaji, hadhi ambayo haijawahi kupingwa hadi leo hii.
3498992
Zenye maoni mengi zaidi