IQNA – Taasisi moja ya mrengo wa kulia nchini Marekani imekiri kuendesha hifadhi ya data (database) yenye maelezo ya maelfu ya Waislamu wa Marekani na mashirika ya Kiislamu kwa takriban miaka ishirini sasa.
Middle East Forum (MEF), shirika lenye utata lililoanzishwa mwaka 1994, limekusanya zaidi ya taarifa milioni 4, zikiwemo majina ya watu, akaunti za mitandao ya kijamii, na taarifa za kodi, pamoja na maelezo ya kina kuhusu misikiti, shule, biashara, na taasisi nyinginezo za Kiislamu. Hifadhi hiyo ya data pia inajumuisha watu na makundi yanayoonekana kuwa washirika wa jamii ya Kiislamu.
MEF ililazimika kufichua kuwepo kwa kumbukumbu hizo baada ya jarida la HuffPost kuihoji shirika hilo kuhusu hifadhi hiyo na kuashiria kuwa lilikuwa na mpango wa kuchapisha ripoti. Kundi hilo limesema litawaruhusu wanazuoni, waandishi wa habari, na watafiti wengine kuomba ruhusa ya kufikia nyenzo hizo.
MEF imedai kuwa dhamira yake ni “kutetea maadili ya Magharibi” na kuangazia kile ilichokitaja kama hatari za “Uislamu wa kisheria” (lawful Islamism). Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za kiraia yamelishutumu kundi hilo kwa kuchochea chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na kusambaza taarifa potofu kuhusu Waislamu.
Ingawa hifadhi hiyo ya data inajumuisha taarifa zilizopatikana kutoka kwenye rekodi za umma, ukubwa wa operesheni hiyo umezua hofu miongoni mwa watetezi wa haki za kiraia.
Caleb Kieffer wa Southern Poverty Law Center ameeleza hifadhi hiyo kuwa ni “ya kusikitisha sana,” akionyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani.
Naye Mobashra Tazamal kutoka Bridge Initiative ya Chuo Kikuu cha Georgetown, ameitaja hifadhi hiyo kuwa “orodha ya walengwa” (target list), akionya kuwa taarifa hizo zinaweza kutumika kufuatilia au kutishia watu na mashirika ya Kiislamu.
Ufichuzi huu unakuja wakati ambapo kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa Waislamu wa Marekani kuhusu chuki dhidi ya Uislamu, sambamba na mivutano ya kisiasa inayozunguka sera za Rais Donald Trump, ukandamizaji wa waandamanaji wanaounga mkono Palestina, na matamshi makali kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama cha Republican.
MEF imejitetea kwa kusema kuwa kufuatilia mitandao ya kiitikadi ni jambo la kawaida miongoni mwa mashirika ya kiraia nchini Marekani, ikidai kuwa makundi mengine nayo yanatunza hifadhi za data kama hizo.
3499005
Zenye maoni mengi zaidi