IQNA

16:26 - September 13, 2026
Habari ID: 3482763

Palestina yapongeza msimamo wa BRICS katika kuunga mkono haki za Wapalestina

IQNA – Palestina imepokea kwa furaha tamko lililotolewa katika mkutano wa viongozi wa BRICS, ikipongeza msimamo wake thabiti wa kuunga mkono haki za watu wa Palestina na harakati za ukombozi wa nchi hiyo.

BRICS

Katika taarifa rasmi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ilipongeza tamko la mkutano wa New Delhi na “misingi na uthibitisho wa msimamo unaounga mkono harakati za Palestina,” hasa kukataa kwa majaribio ya kuwafukuza Wapalestina kwa nguvu kutoka kwenye ardhi yao, ikiwa ni pamoja na Al-Quds. Tamko hilo pia limehimiza kukomesha utawala wa Kizayuni, na kuunga mkono kujiunga kwa Dola ya Palestina kikamilifu katika Umoja wa Mataifa.

Aidha, Wizara hiyo imepongeza msimamo wa tamko hilo la kuunga mkono shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina (UNRWA) na mamlaka yake, pamoja na wito wa kulinda maeneo matakatifu na kuhakikisha ufikiaji wa maeneo hayo jijini Al-Quds, kulinda watu wa Palestina, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika bila kikwazo katika Ukanda wa Gaza.

Wizara hiyo ilisema kuwa msimamo huo unaendana na sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, na ilisisitiza hitaji la kuugeuza msimamo huo kuwa hatua madhubuti na za vitendo.

Iliimiza jumuiya ya kimataifa “kuchukua majukumu yake ya kisheria na kisiasa, na kufanya kazi katika kutekeleza na kusimamia maazimio ya uhalali wa kimataifa” ili kuhakikisha mwisho wa uhalifu na ukiukaji wa sheria unaofanywa na utawala wa Kizayuni, pamoja na aina zote za ubaguzi, upanuzi wa makazi ya wakoloni, na unyakuzi wa ardhi, huku ikilinda watu wa Palestina na kuwaruhusu kutumia haki zao halali za kitaifa, ambapo haki kuu ni ile ya kujiamulia mambo wenyewe.

Wizara hiyo ilisisitiza kuwa “utekelezaji wa msimamo na uthibitisho uliomo katika tamko la BRICS unahitaji kukomesha utawala wa Kizayuni na kuwaruhusu Wapalestina kutumia haki zao ambazo haziwezi kunyang’anywa,” ikiwemo kuanzishwa kwa Dola huru na yenye mamlaka ya Palestina katika ardhi yake, ikiwa Al-Quds ndiyo mji mkuu wake.

Mapema siku ya Jumamosi, tamko la mwisho lililotolewa mwishoni mwa mkutano wa viongozi wa BRICS lilionyesha upinzani mkali dhidi ya jaribio la kuwafukuza Wapalestina kwa nguvu kutoka Gaza na Ukingo wa Magharibi uliokaliwa kinyume cha sheria.

Tamko hilo lilitoa wito wa suluhu ya haraka na ya kudumu kwa suala la Palestina na kuthibitisha tena uungaji mkono wake kwa Dola ya Palestina kupata wanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Kikundi cha BRICS kinajumuisha wanachama wa muda mrefu: Brazil, Urusi, India, China, na Afrika Kusini,  ambako jina la BRICS linatokana , pamoja na wanachama wapya: Misri, Ethiopia, Indonesia, Iran, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kupitia upanuzi wake hadi kuwa wanachama 11 tangu mwaka 2024, BRICS imekuwa kundi linalowakilisha takriban nusu ya idadi ya watu duniani na takriban asilimia 40 ya uzalishaji wa uchumi wa dunia.

3499003

Habari zinazohusiana
Kishikizo: BRICS palestina
captcha