IQNA – Kwa Waziri wa Masuala ya Dini wa Indonesia, Prof. Nasaruddin Umar, Musabaqa ya 31 ya Kitaifa ya Qiraa na Kuhifadhi Qur’ani Tukufu (MTQ), inayoendelea hivi sasa katika jimbo la Java ya Kati, ina lengo pana na tukufu zaidi kuliko kushinda mataji tu , inalenga kupanda na kulea mwenendo na tabia yenye misingi ya Kiqur’ani maishani.
“Qur’ani Tukufu iliteremshwa ili isomwe, ieleweke, na ujumbe wake uzingatiwe na kufanyiwa kazi,” alisema waziri huyo wakati akifungua rasmi mashindano hayo ya 31 ya kitaifa katika Uwanja wa Simpang Lima, jijini Semarang, siku ya Jumamosi.
Alieleza kuwa katika ngazi ya familia, mwenendo wa Kiqur’ani hudhihirika kupitia mapenzi, kuwajibika, mashauriano (shura), na kulindana heshima na hadhi ya kila mmoja.
“Hakuna ukatili, matusi, wala maamuzi ya mabavu yanayoweza kuhalalishwa kwa jina la dini,” alisisitiza.
Akiangazia mazingira ya ofisini na sehemu za kazi, aliendelea kueleza kuwa tabia ya Kiqur’ani hujidhihirisha katika uaminifu, nidhamu, weledi, na utoaji wa haki bila upendeleo.
“Qur’ani haipaswi kusikika tu wakati wa ufunguzi wa shughuli na hafla, kisha athari zake zikatoweka pindi tunaposimamia bajeti, tunapotumia mamlaka, tunapotoa huduma, au tunapofanya maamuzi,” alisema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watu walio karibu zaidi na Qur’ani ndio wanaopaswa kuwa waaminifu zaidi, wenye bidii kubwa kazini, na walio mbali kabisa na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
“Katikati ya jamii, tabia hii ya Kiqur’ani hutekelezwa kupitia misingi ya Ta’aruf (kufahamiana), Ta’awun (kusaidiana katika mambo ya kheri), na Tabayyun (kuhakiki habari kabla ya kuieneza),” aliongeza.
Alibainisha kuwa msimamo halisi wa Kiqur’ani ni kukataa uzushi na kashfa (fitna), habari za upotoshaji, kauli za chuki, na vitendo vyote vinavyoharibu heshima ya mtu na kuvunja udugu.
Katika muktadha wa taifa na serikali, alisema kuwa kuwa na mwenendo wa Kiqur’ani kunamaanisha kusimamisha uadilifu, kulinda umoja, kutetea na kuwahami wanyonge na waliokandamizwa (mustadh’afin), kuheshimu utofauti, na kutanguliza maslahi ya wote mbele.
“Kadiri mtu anavyokuwa karibu zaidi na Qur’ani, ndivyo tabia na maadili yake yanavyopaswa kuwa ya kiungwana na matukufu zaidi, kauli zake kuwa zenye staha, heshima yake kwa mitazamo tofauti kuongezeka, na mchango wake kuwa mkubwa zaidi katika kuleta maelewano na mshikamano wa kitaifa,” alisema.
Musabaqa hiyo ya 31 ya MTQ inafanyika kuanzia Septemba 11 hadi 20, 2026, huku mashindano yakirindima katika viwanja na kumbi 12 zilizotawanyika katika mji mzima wa Semarang.
Jumla ya washiriki 2,242, wakijumuisha washiriki wakuu 1,751 na washiriki wa akiba 491, wanachuana katika vitengo vinane na makundi 24 ya mashindano yaliyo chini ya kategoria 48.
3499002
Zenye maoni mengi zaidi