IQNA – Mwalimu mmoja wa kike Muislamu katika jimbo la East Flanders nchini Ubelgiji amefutwa kazi kwa uonevu baada ya kukataa kusalimu amri mbele ya sheria inayopiga marufuku alama za kidini katika shule za jimbo hilo, akisisitiza haki yake ya kimsingi ya kuvaa vazi la staha la Hijabu.
Serikali ya jimbo la East Flanders imemfuta kazi mwalimu huyo, kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la utangazaji la VRT siku ya Jumatatu.
Mwalimu huyo, Bi. Hadija Amajoud, ambaye amekuwa akifundisha katika shule ya serikali ya mahitaji maalum katika mji wa Assenede tangu mwaka 2022, alikuwa akivaa Hijabu yake tangu alipoanza kazi katika kituo hicho cha elimu.
Hata hivyo, hatua za kinidhamu zilichukuliwa dhidi yake mara tu Bi. Amajoud alipoweka wazi msimamo wake thabiti kuwa hana nia wala hatakubali kuvua vazi lake la heshima la Hijabu wakati akiwa darasani akitekeleza wajibu wake wa kutoa elimu.
Chama cha Wafanyakazi cha ACOD kimetangaza nia yake ya kupinga vikali uamuzi huo wa kufukuzwa kazi mbele ya Mahakama ya Rufaa mjini Brussels. Chama hicho kilibainisha kuwa kesi hiyo inabeba uzito mkubwa na inaweza kuweka kigezo muhimu cha kisheria kuhusu uhuru wa kuabudu na dhana tata ya “kutopendelea upande wowote” katika sekta ya elimu.
Bi. Amajoud alipinga vikali hatua hiyo na kuhoji mipaka ya mwajiri katika kuingilia na kubana uhuru binafsi na wa kiitikadi wa mwalimu, huku akitaja tafsiri ya utawala wa jimbo hilo kuhusu dhana ya “kutopendelea” kuwa ni “mbinu ya kisiasa tupu inayotumika kukandamiza haki za kidini.”
“Kimsingi, hakuna mwanadamu asiyekuwa na msimamo au upande. Kila mwalimu anaposimama mbele ya darasa huwa na itikadi na miongozo yake ya kimaadili,” alisisitiza Bi. Amajoud.
Kwa upande wake, utawala wa jimbo ulijitetea ukidai kuwa ulikuwa unalazimika kutekeleza kanuni za watumishi zilizopitishwa kile walichokiita “mchakato wa kidemokrasia.”
Marufuku hiyo dhidi ya nembo za kidini na kisiasa imekuwa ikitekelezwa katika shule zote zinazosimamiwa na jimbo hilo tangu kuanza kwa mwaka huu wa masomo.
Chini ya sheria hizo zenye ubaguzi, walimu na wanafunzi wanapigwa marufuku kuvaa beji, alama, au mavazi yoyote yanayoakisi msimamo wa kisiasa au wa kiimaniو hatua ambayo kimsingi inalenga kumnyima mwanamke wa Kiislamu fursa za kimaisha kwa sababu ya vazi lake la kidini.
Hapo awali, wanafunzi sita pamoja na mashirika kadhaa ya kiraia walipinga kanuni hiyo dhalimu mbele ya Baraza la Taifa la Ubelgiji, lakini mahakama hiyo ilitupilia mbali madai yao mwezi Mei uliopita.
Hata hivyo, Taasisi ya Haki za Binadamu ya Flemish ilikuwa imekwisha thibitisha mapema kuwepo kwa mazingira ya ubaguzi wa wazi na vitisho katika kadhia hiyo ya Bi. Amajoud.
3499028
Zenye maoni mengi zaidi