IQNA – Katika hatua inayoangazia kukithiri kwa chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na vitendo vya uhasama katika jamii ya Uingereza, vituo vipya vya kuripoti jinai na mashambulizi ya chuki vimeanzishwa ndani ya misikiti nchini humo, kwa lengo la “kuvunja vikwazo” vilivyowazuia Waislamu wengi kujitokeza, kwa kuwapa mazingira salama na yanayoaminika kuripoti madhila wanayokumbana nayo.
“Kama jamii, kwa miaka mingi tumekuwa tukiambiwa: ‘Lazima muwe wavumilivu zaidi. Ninyi ni wageni tu katika nchi hii; hamtatendewa kwa usawa kamwe,’” alieleza Faisal Mahmood, mmoja wa viongozi wa jamii kutoka Peterborough, akisimulia maumivu ya malezi na maisha ya Muislamu nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa Mahmood, hisia hizi zilizojengeka kwa kina na kupandikizwa kiakili ndizo zilizopelekea wahanga wengi kutotoa taarifa za mashambulizi ya chuki wanayofanyiwa. Alieleza kuwa kwa muda mrefu, lugha za kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu zilikuwa zikimezwa na kuvumiliwa na wahanga kama jambo la “kawaida lililozoeleka,” hali iliyozusha pengo kubwa katika takwimu rasmi za serikali, jambo ambalo sasa linapaswa kubadilika.
Jeshi la Polisi la Cambridgeshire lilisema kuwa takriban matukio 600 ya jinai za chuki (ya aina zote) yalirekodiwa katika mji wa Peterborough kati ya Agosti 2025 na Agosti 2026. Hata hivyo, ili kurahisisha utoaji wa taarifa, vituo hivyo vya kuripoti vimewekwa katika misikiti mitatu ya mji huo kama sehemu ya mpango huo mpya.
Mahmood, ambaye ni Katibu wa Baraza la Pamoja la Misikiti, alibainisha kuwa vituo hivi vitaondoa kipingamizi cha woga na kuifanya iwe “rahisi na salama zaidi kwa wahanga ndani ya jamii kujitokeza.”
Vituo hivyo vimewekwa katika Msikiti wa Faizan-e-Madina uliopo Mtaa wa Gladstone, Msikiti wa Bibi Khadijah uliopo Cromwell Road, na Kituo cha Jamii ya Wakurdi huko Woodston. Katika maeneo haya, askari polisi wamewafunza wafanyakazi wa kujitolea jinsi ya kutambua matukio yanayochochewa na chuki, kuelewa mifumo rasmi ya kisheria ya utoaji taarifa, na kuwaelekeza wahanga kwenye huduma stahiki za msaada na hifadhi.
Mahmood aliongeza kuwa matukio ya kijamii na kisiasa nchini humo katika miaka michache iliyopita yameiacha jamii ya Kiislamu ikiwa katika “hali ya hatari na wasiwasi mkubwa,” huku baadhi ya waumini wakilazimika “kujifungia ndani ya nyumba zao” kwa hofu ya kushambuliwa.
Mnamo mwaka 2024, misikiti katika mji huo ililazimika kupunguza masaa ya kufungua milango yake baada ya wimbi kubwa la ghasia za kigaidi za mrengo wa kulia wenye msimamo mkali (far-right) kuzuka kote nchini Uingereza, kufuatia tukio ambapo wasichana watatu walidungwa visu na kuuawa na kijana wa miaka 17 huko Southport, ghasia zilizoelekezwa kimakusudi kushambulia jamii za Kiislamu na nyumba za ibada kwa uchochezi wa vyombo vya habari vya Magharibi.
Mwezi Desemba mwaka huo, Alexander Hooper wa Dogsthorpe Road alihukumiwa kifungo cha wiki 27 jela, kilichosimamishwa kwa miezi 18 (suspended sentence), baada ya kukiri kutenda kosa lililochochewa na chuki za kidini na ubaguzi wa rangi dhidi ya Msikiti wa Darassalaam.
Akirejelea ghasia hizo za mwaka 2024, Mahmood alisema: “Nilikuwa na wasiwasi mkubwa; wakati vurugu hizo zikiendelea, niliposimama kwenye vituo vya treni za chini ya ardhi, nilikuwa nikifikiria: Sitaki mtu aninyeshe ama anirushe reli. Kwa hiyo nilikuwa nikiegama ukutani kwa tahadhari kubwa.”
Aliongeza: “Lakini tumezoea hali hii kwa miaka mingi. Mtu anapotoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu au ya kibaguzi, unalazimika kumeza na kukubali ukidhani ndivyo maisha yalivyo. Lakini tusipobadilisha hilo sasa, unyanyasaji huu utaendelea daima.”
Mahmood alibainisha kuwa jamii imeipokea hatua ya vituo hivyo kwa shauku na mwelekeo chanya. Hatua hii imekuja baada ya Baraza la Jiji la Peterborough kupitisha azimio rasmi kuhusu chuki dhidi ya Uislamu mwaka jana, likijumuisha ufafanuzi wa kina wa ‘Islamophobia’ na kuainisha jinsi Waislamu wanavyoathiriwa kisaikolojia na kijamii.
Akifafanua athari pana za vitendo hivi vya chuki, ambazo zinavuka mashambulizi ya kimwili, Mahmood alisisitiza: “Mwanamke wa Kiislamu anapojitokeza akiwa amevaa Hijabu yake ya heshima, suala si tu kuvuliwa Hijabu hiyo kwa nguvu za kimwili; bali anapofanywa ajihisi kuwa yeye hastahili kuwepo mahali hapo kwa sababu tu ya vazi lake la staha, hiyo yenyewe ni chuki ya wazi dhidi ya Uislamu.”
“Ninaamini tunapaswa kuishi katika jamii inayoheshimu na kuvumilia itikadi tofauti za watu… tunapaswa kujifunza kuishi pamoja kwa manufaa na mustakabali wa vizazi vijavyo na nchi yetu.”
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Cambridgeshire alikaririwa akisema: “Tuna mifumo imara ya kuchunguza jinai za chuki ili kuhakikisha zinarekodiwa ipasavyo na kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria na miongozo ya kitaifa. Ikiwa kuna makundi mengine ya kidini au ya kijamii yanayotaka kushirikiana nasi kuwa vituo vya kuripoti mashambulizi ya chuki, yanakaribishwa kuwasiliana nasi.”
/3499023
Zenye maoni mengi zaidi