IQNA – Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, Hujjatul-Islam Sheikh Ibrahim Zakzaky, ametoa onyo zito kwa Waislamu dhidi ya mitego ya migogoro na migawanyiko ya ndani, akisisitiza kuwa hitilafu hizo zinatumiwa kimakusudi na maadui wa Uislamu ili kulidhoofisha taifa la Kiislamu na kulipotosha kutoka kwenye vipaumbele vyake vya kimsingi.
Sheikh Zakzaky alikazia wajibu wa kisheria na wa kimaadili wa kudumisha umoja miongoni mwa Waislamu wote, akiutaka umma kurejea kwenye mafundisho asilia na sahihi ya Uislamu yaliyoletwa na Mtume wa Rehma, Muhammad Mustafa (SAW).
“Mtume Mtukufu (SAW) alikuja na dini iliyokamilika na kamilifu, na juu ya msingi huo imara alijenga Umma thabiti. Wajibu wetu mkuu leo ni kufuata njia hiyo bila kupotoka,” alibainisha kiongozi huyo wa mapambano ya Kiislamu barani Afrika.
Sheikh Zakzaky aliongeza kuwa kambi ya maadui wa Uislamu na mabeberu inafanya kila iwezalo kuchafua shakhsia tukufu na adhama ya Mtume wa Rehma (SAW), kwa kuwa wanatambua fika kuwa Mtume ndiye nguzo kuu na alama ya kipekee ya mshikamano na umoja usiovunjika wa Waislamu ulimwenguni kote.
Kadhalika, alionya vikali dhidi ya fitina na migogoro inayochochewa kimakusudi miongoni mwa Waislamu, akifafanua kuwa mivutano ya kimadhehebu, kidini au kikabila haina tija yoyote kwa masilahi ya Umma wa Kiislamu.
Kwa mujibu wa Sheikh Zakzaky, mizozo hiyo hutumikia na kunufaisha masilahi ya wale walioibuni, wanaoifadhili na kuiongoza nyuma ya pazia kwa ajili ya kufanikisha malengo yao ya kikoloni.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu alisisitiza kuwa madola ya kibeberu na vibaraka wao huchochea mapigano, ukosefu wa usalama na chuki za ndani ili kughafirisha na kupumbaza fikra za wananchi, wakati wao wakiendelea kupora utajiri na maliasili za jamii hizo, hali inayozidisha umaskini uliokithiri na kuimarisha mifarakano miongoni mwa watu.
Amehitimisha kwa kueleza kuwa kutambua na kuzifichua mbinu hizi ovu za maadui, kuimarisha ngome ya umoja ndani ya Umma, na kurejea kwenye mafundisho halisi ya Mtume wa Rehma (SAW) ndizo hatua za lazima na za msingi katika kukabiliana na changamoto zote zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu hivi leo.
3499026
Zenye maoni mengi zaidi