IQNA

15:36 - September 21, 2026
Habari ID: 3482801

Siku ya Amani Duniani: Njozi ya Ulimwengu Chini ya Kivuli cha Vita vya Marekani na Israel

IQNA – Siku ya Amani Duniani, inayoadhimishwa kila Septemba 21, mwaka huu inakuja wakati ulimwengu ukikabiliwa na mfululizo wa vita na migogoro ya kiusalama inayozidi kuenea, huku Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ikiwa tena katika kitovu cha wasiwasi wa kimataifa.

s

Septemba 21 huadhimishwa na Umoja wa Mataifa kama Siku ya Kimataifa ya Amani, siku iliyokusudiwa kusisitiza moja ya kanuni za msingi za jumuiya ya kimataifa: kuzuia vita, kukataa vitendo vya kikatili, na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.

Hata hivyo, maadhimisho ya mwaka huu yanakuja katika wakati ambapo pengo kati ya matamanio ya amani na uhalisia wa mambo linabaki kuwa kubwa na la kutisha. Migogoro ya kivita inaendelea katika maeneo kadhaa, huku Mashariki ya Kati ikishuhudia ongezeko kubwa la mivutano kufuatia vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, sambamba na janga la kibinadamu lililosababishwa na utawala katili wa Israel huko Gaza.

Kutoka Azimio la Umoja wa Mataifa hadi Ishara ya Kimataifa

Wazo la kutenga siku kwa ajili ya amani lilianzishwa kwa mara ya kwanza na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1981.

Tarehe 30 Novemba ya mwaka huo, Baraza Kuu lilipitisha Azimio namba 36/67, likianzisha Siku ya Kimataifa ya Amani. Maadhimisho ya kwanza yalifanyika Septemba 1982.

Awali, siku hiyo haikuwa na tarehe maalumu na ilihusishwa na ufunguzi wa kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hali hiyo ilibadilika mnamo mwaka 2001.

Tarehe 7 Septemba 2001, Baraza Kuu lilipitisha Azimio namba 55/282, likiweka tarehe 21 Septemba kuwa tarehe rasmi na ya kudumu ya Siku ya Kimataifa ya Amani, na kuitangaza kuwa siku iliyotengwa kwa ajili ya kuimarisha misingi ya amani na kusitisha uhasama kote ulimwenguni.

Tangu wakati huo, Septemba 21 imekuwa ukumbusho wa kila mwaka wa haja ya kuzuia migogoro ya kivita na kutatua mizozo ya kimataifa kupitia diplomasia na mazungumzo.

Hata hivyo, zaidi ya miongo minne tangu azimio la kwanza la Umoja wa Mataifa, umbali kati ya azma hiyo na uhalisia wa siasa za kimataifa unasalia kuwa mkubwa.

Amani katika Mashariki ya Kati: Kati ya Vita na Diplomasia Iliyofeli

Mashariki ya Kati inasalia kuwa moja ya mifano dhahiri ya utata huu.

Uchokozi ulioanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28, 2026 umezua tena maswali ya msingi kuhusu uwezo wa taasisi za kimataifa kuzuia vita na kulinda raia.

Gaza: Amani Ambayo Bado Haijakomesha Vita

Gaza inawakilisha mtihani mwingine mkubwa kwa dhamira ya kimataifa ya amani. Utawala wa Israel ulianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo la Palestina Oktoba 2023 na hadi sasa utawala huo umeua Wapalestina wasipungua 73,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Licha ya mipango ya kusitisha mapigano na juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kumaliza mgogoro, vitendo vya kikatili na mauaji ya raia yameendelea.

Madhara ya kibinadamu ya vita hivyo yamekuwa ya kuhuzunisha sana. Idadi kubwa ya Wapalestina wameuawa shahidi au kujeruhiwa, huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na ukimbizi, uharibifu wa miundombinu, na hali ngumu ya kibinadamu.

Msaada wa kijeshi unaoendelea kutolewa na Marekani kwa Israel pia umesalia kuwa hoja kuu ya mjadala wa kimataifa.

Washington imeendelea kuipatia Israel vifaa vya kijeshi hata wakati ambapo mashirika ya kimataifa na makundi ya kibinadamu yameonyesha wasiwasi wao kuhusu kiwango cha mateso ya raia huko Gaza.

Kwa waangalizi wengi, mgogoro wa Gaza umekuwa mtihani si tu wa dhamira ya jumuiya ya kimataifa kuelekea amani, bali pia wa ufanisi wa sheria za kimataifa za kibinadamu na taasisi zilizoundwa kulinda raia wakati wa migogoro ya kivita.

Wakati Vita Vinapochukua Nafasi ya Diplomasia

Siku ya Amani Duniani si hafla ya ishara tu. Kanuni yake kuu ni kwamba mizozo ya kimataifa inapaswa kushughulikiwa kupitia majadiliano, upatanishi, na mbinu za kisheria kabla ya kugeuka kuwa migogoro ya kivita.

Hata hivyo, uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umeonyesha kuwa nguvu ya kijeshi inasalia kuwa nyenzo kuu ya sera za kigeni kwa madola makubwa.

Vitendo vya Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati vimekuwa sehemu muhimu ya mjadala mpana kuhusu mustakabali wa amani na usalama wa kimataifa. Wakosoaji wanasema kuwa kutegemea mara kwa mara nguvu za kijeshi kunahatarisha kupanua migogoro na kudhoofisha juhudi za kidiplomasia, huku watawala wa Washington na Tel Aviv wakiwasilisha vitendo vyao vya kijeshi kama hatua za lazima kwa ajili ya usalama na uzuiaji.

3499097

Habari zinazohusiana
captcha