IQNA

15:53 - September 21, 2026
Habari ID: 3482803

Mwanasosholojia: Mtume Muhammad (SAW) ni mfano usio na kifani wa kusimama na wananchi

IQNA – Mtume Muhammad (SAW) alionyesha ukaribu wake na watu kwa kushiriki binafsi katika ujenzi wa Msikiti wa Quba, akibeba mawe mazito bega kwa bega na Waislamu wengine licha ya ugumu wa safari yake kutoka Makka, anaeleza mwanasosholojia na mtaalamu wa dini wa Iran.

quba

Hujjatul Islam Alireza Qobadi amesisitiza mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW) wakati wa kukaa kwake Quba baada ya Hijra kutoka Makka kwenda Madina, akiuelezea kama mfano wa uongozi kupitia vitendo.

Baada ya Mtume Muhammad (SAW)  kufika Quba, kazi yake kuu ya kwanza ilikuwa ujenzi wa msikiti. Licha ya kuwa ametoka tu kukamilisha safari ngumu kutoka Makka, aliamuru msikiti huo ujengwe. Baada ya ardhi kupatikana, Mtume alijiunga na watu katika kuujenga.

Hujjatul Islam Qobadi ameliambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) kuwa nafasi na hadhi tukufu ya Mtume Muhammad (SAW)  haikumtenga na watu wakati wa kazi hiyo. Badala ya kujizuia na kazi ndogo, alijitwika kazi ngumu, ikiwa ni pamoja na kubeba mawe makubwa, kana kwamba alichukulia kazi hiyo kama jukumu lake binafsi.

Msomi huyo ameashiria riwaya au simulizi kutoka kwa mmoja wa Ansar aliyemuona Mtume Muhammad (SAW) akibeba jiwe kubwa. Mtu huyo alimwendea ili amchukue jiwe hilo na kulibeba yeye, lakini Mtume Muhammad (SAW)  alikataa na kumwambia, “Nenda mwenyewe ukabebe jiwe kama hilo nililolibeba.”

Kulingana na Qobadi, ushiriki wa Mtume Muhammad (SAW)  uliwapa moyo mkubwa Waislamu waliokuwa wakifanya kazi katika msikiti huo na kuonyesha kuwa yeye alikuwa kiongozi aliye mstari wa mbele katika kutekeleza mafundisho ya Kiislamu.

“Ingawa alikuwa msafiri na ilikuwa ni busara kwa watu kutarajia asimamie tu ujenzi wa msikiti, hakufanya hivyo,” amesema Hujjatul Islam Qobadi. “Kupitia mwenendo kama huu, Mtume Muhammad (SAW)  alionyesha kuwa yeye alikuwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mafundisho ya Kiislamu.”

Aliongeza kuwa mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW)  ulikuwa na athari kubwa kwa utayari wa watu kufuata mfano wake, ukiimarisha mapenzi na utiifu wao kwake, wakati huo huo ukisaidia kazi ya ujenzi kusonga mbele kwa haraka na kwa uimara.

Hujjatul Islam Qobadi amesema watu wenyewe walitambua umuhimu wa Mtume Muhammad (SAW)   kufanya kazi pamoja nao  hivyo huo ni mfano usio na kifani wa kusimama pamoja na kushirikiana na watu moja kwa moja kivitendo katika kazi ngumu ya ujenzi wa msikiti. 

3499105

captcha