IQNA – Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), ambalo ni shirika kubwa zaidi nchini humo la kutetea haki za kiraia na masilahi ya Waislamu, limakaribisha hatua ya kufunguliwa mashtaka dhidi ya mwanamume mmoja kutoka Kaunti ya Spotsylvania, huko Virginia, kuhusiana na tishio la kuweka bomu lililolenga Kituo cha Kiislamu cha All Dulles Area Muslim Society (ADAMS Center).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Loudoun, vyombo vya sheria vilimkamata Adam Sawyer mwenye umri wa miaka 50 mnamo Septemba 19, kufuatia uchunguzi kuhusu maoni yaliyowekwa kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa Kituo cha ADAMS. Maoni hayo yalionyesha nia ya kufikisha kifaa cha kulipuka katika hafla iliyoandaliwa na msikiti huo. Sawyer amefunguliwa mashtaka rasmi ya kosa moja la kutoa vitisho vya kulipua.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kitaifa wa CAIR, Nihad Awad, alisema:
“Tunakaribisha hatua ya haraka na ya ushirikiano iliyochukuliwa na Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Loudoun, Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Spotsylvania, Jeshi la Polisi la Jimbo la Virginia, na Idara ya Polisi ya Kaunti ya Fairfax katika kumtambua na kumtia mbaroni mtuhumiwa katika kesi hii ya kutisha. Vitisho vinavyolenga nyumba za ibada vinagusa misingi mikuu ya uhuru wa kuabudu na usalama wa umma. Tunazisihi mamlaka za kisheria kuzingatia mashtaka yanayofaa ya jinai za chuki endapo ushahidi utadhihirisha nia iliyochochewa na ubaguzi, na tunazishauri taasisi zote za Kiislamu kusalia macho na kuimarisha itifaki thabiti za kiusalama.”
CAIR inatoa wito kwa viongozi wa jamii ya Kiislamu kutumia rasilimali zake za sasa kusaidia kuweka salama vituo vya ibada. Mapema Jumatatu hiyo hiyo, tawi la CAIR katika jimbo la Michigan lilikaribisha pia mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya mwanamke mmoja kutoka Roseville ambaye anadaiwa kutishia kufanya ghasia dhidi ya msikiti wa eneo hilo na Meya wa Dearborn, Abdullah Hammoud.
Ripoti ya hivi karibuni ya haki za kiraia iliyotolewa na CAIR ilirekodi malalamiko 8,683 ya ubaguzi dhidi ya Waislamu kwa mwaka wa 2025, ikiwa ni idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa na shirika hilo tangu lianze kuchapisha ripoti za haki za kiraia mwaka 1996.
Hivi karibuni, CAIR yenye makao yake makuu mjini Washington, D.C., ilitangaza kuwa imerekodi matukio 17 yaliyolenga nyumba za ibada za Kiislamu katika miezi ya Mei, Juni, na Julai mwaka huu pekee. Matukio hayo 17 yanawakilisha asilimia 51 ya jumla ya matukio ya mwaka uliopita, na ongezeko la asilimia 183 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha miezi mitatu mwaka jana, ambapo CAIR ilirekodi matukio sita ya namna hiyo.
3499126