IQNA

17:56 - September 23, 2026
Habari ID: 3482811

Rais wa Austria aikosoa vikali Israel kwa kufanya jinai za kivita na kukiuka sheria za kimataifa

IQNA – Rais wa Austria amekosoa vikali utawala wa Kizayuni kwa kufanya jinai za kivita dhidi ya Wapalestina na kukiuka sheria za kimataifa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne mjini New York akiandamana na Kansela wa Shirikisho Christian Stocker na Waziri wa Mambo ya Nje Beate Meinl-Reisinger, pembezoni mwa kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Austria Alexander Van der Bellen alisema kuwa vitendo vya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na ni jinai za kivita.

Alitaja hasa suala la kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, akionya kuwa Tel Aviv inafuata “mwelekeo hatari.”

Rais huyo wa Austria aliongeza kuwa mambo yanayoendelea kwa sasa katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavuhayataleta maslahi yoyote kwa Israel kwa muda mrefu, akibainisha kuwa jamii ya kimataifa inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kuhusu suala la kuheshimu sheria za kimataifa na mfumo uliopo wa kimataifa.

Kauli za Van der Bellen zimetolewa pembezoni mwa ushiriki wa viongozi wa Austria katika wiki ya ngazi ya juu ya kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huku Austria ikijiandaa kuchukua kiti cha kura isiyo ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2027–2028.

Awali, Kansela wa Austria Christian Stocker alieleza Umoja wa Mataifa kuwa “kitovu cha diplomasia na ushirikiano wa kimataifa,” akibainisha kuwa uanachama ujao wa Austria katika Baraza la Usalama unawakilisha jukumu kubwa kwa jamii ya kimataifa.

3499139

Habari zinazohusiana
Kishikizo: austria palestina
captcha