IQNA – Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika hatua ya kulaani kile ilichokitaja kama kitendo cha kigaidi kisichokubalika, limetoa tamko la kulaani shambulio la kigaidi la kujitoa muhanga katika msikiti mmoja kaskazini-magharibi mwa Pakistan, shambulio lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 24 na kujeruhi makumi ya wengine.
“Wajumbe wa Baraza la Usalama wamelaani kwa maneno makali zaidi shambulio la kigaidi la kinyama na la woga la kujilipua katika msikiti mmoja huko Kohat, Mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, nchini Pakistan,” ilisema taarifa iliyotolewa na Rais wa Baraza hilo, Jerome Bonnafont wa Ufaransa.
Shambulio hilo la Septemba 18 lilisababisha vifo vya Wapakistani wasiopungua 24, wakiwemo raia saba na maafisa 17 wa vyombo vya usalama, na kuacha angalau watu 88 wakiwa wamejeruhiwa. Kundi moja la wanamgambo wenye mfungamano na Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) limedai kuhusika na shambulio hilo.
Wajumbe wa Baraza hilo wamesisitiza umuhimu mkubwa wa kuwawajibisha “wahusika, waandaaji, wafadhili, na wale wanaounga mkono” vitendo hivyo, wakizihimiza nchi zote kushirikiana kikamilifu na serikali ya Pakistan kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio husika ya Baraza hilo.
Wakati wakieleza masikitiko yao ya dhati na kutoa rambirambi kwa familia za waathiriwa na wananchi wa Pakistan, Baraza hilo limethibitisha tena kuwa ugaidi unasalia kuwa “mojawapo ya tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa,” na kusisitiza kuwa vitendo hivyo ni vya “kihalifu na visivyoweza kuhalalishwa, bila kujali nia yake, mahali popote, wakati wowote, na yeyote anayefanya.”
3499133