IQNA

20:59 - September 24, 2026
Habari ID: 3482813

“Iran ni Mwathiriwa wa Ugaidi,” asema Rais Pezeshkian katika hotuba UNGA

IQNA – Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa nchi yake ni mwathiriwa wa ugaidi na imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya kikatili ambayo yamesababisha kuuawa shahidi kwa Kiongozi Muadhamu, raia wasio na hatia, pamoja na uharibifu wa miundombinu muhimu.

unga

Akihutubia kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York siku ya Jumatano, Pezeshkian alijibu tuhuma zilizoelekezwa dhidi ya Iran na Rais wa Marekani Donald Trump, huku akibainisha wazi misimamo ya Tehran kuhusu masuala ya ulinzi, nishati ya nyuklia, usalama wa kikanda, kadhia ya Palestina, sheria za kimataifa, na mazungumzo.

Rais Pezeshkian alieleza kuwa Iran imekabiliwa na mfululizo wa mashambulizi yalipelekea kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu na raia wa kawaida pamoja na kuharibiwna miundombinu ya kitaifa. Alibainisha kuwa shule, vituo vya michezo, hospitali, vyuo vikuu, madaraja, na miundombinu mingine muhimu imekuwa ikilengwa na mashambulizi hayo ya kigaidi.

Akiashiria shambulio la kikatili katika ukumbi wa michezo huko Lamerd, Rais alisema watoto na vijana walikuwepo katika eneo hilo wakati wa tukio, na watu wasio na hatia walipoteza maisha. Alisisitiza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia silaha za Marekani na Israel, huku akionyesha kusikitishwa na hatua ya wale wanaofadhili na kutekeleza ugaidi kuigeuzia Iran tuhuma za kuwa eti ni nchi ya kigaidi.

Sisi si magaidi

“Sisi si magaidi; sisi ni waathiriwa wa ugaidi,” alisisitiza Rais Pezeshkian, akiongeza kuwa hatua zote za kijeshi zinazochukuliwa na Iran zinatekelezwa kwa misingi ya kujihami na kulinda mamlaka ya taifa.

Alisema kuwa Marekani na utawala ghasibu wa Kizayuni wameishambulia Iran kwa silaha na teknolojia za kisasa kabisa, ilhali Jamhuri ya Kiislamu imejihami na kujilinda bila ya kuwalenga raia kwa namna yoyote ile. Kadhalika, alitaja mauaji ya kigaidi ya aliyekuwa kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Shahidi Ismail Haniyeh, yaliyofanyika mjini Tehran muda mfupi tu baada yeye (Pzeshkian)  kuapishwa kama Rais na kuanza rasmi majukumu yake, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vya kinyama vinakiuka waziwazi sheria na mikataba ya kimataifa.

Pezeshkian alieleza kuwa uzoefu wa mashambulizi ya hivi karibuni umeimarisha imani ya Iran kwamba nchi yoyote isiyoweza kujilinda na kujihami yenyewe itasalia kuwa dhaifu na inayoweza kushambuliwa wakati wowote.

Iran inahitaji uwezo wa kijeshi kujilinda

Alibainisha kuwa Iran inahitaji nguvu za kijeshi kwa ajili ya kujilinda na si kwa ajili ya uchokozi wala uvamizi, akiongeza kuwa uwezo wake wa kiulinzi unakusudiwa kuhakikisha uhai, usalama, na maendeleo endelevu ya nchi. Alitanabahisha kuwa Iran haijawahi kuivamia wala kuishambulia nchi yoyote ile kwa zaidi ya miaka 200, akifafanua mkakati wake wa kijeshi kuwa umejengwa juu ya misingi thabiti ya kujilinda na kuzuia uchokozi (nguvu ya uzuiaji/ deterrence).

Aidha, Pezeshkian alizungumzia mchango mkubwa na wa kihistoria wa wananchi wa Iran katika kuitetea na kuilinda nchi yao, akisema walisimama imara katika medani na mabarabarani kwa muda wa miezi saba ili kuitunza nchi na kuzuia njama zote zilizolenga kuzusha machafuko na kuvuruga usalama wa ndani.

“Wananchi ndio chimbuko la nguvu zetu,” alisema Rais, akiongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kuwa thabiti na yenye nguvu za kutosha ili kuhakikisha uhai na ustawi wake; iwe yenye hekima na uwajibikaji ili isitumie nguvu zake kuwakandamiza wengine; na iwe yenye maono mapana ya mbali kiasi cha kutotafuta usalama wake kwa njia ya kuvuruga usalama wa nchi jirani.

Rais Pezeshkian alisisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran umejikita katika malengo ya amani ya kimaendeleo, na wala si kwa ajili ya uzalishaji wa silaha za maangamizi. Alifafanua kuwa teknolojia ya nyuklia ni haki ya kimsingi ya Iran ya kujiletea maendeleo, akibainisha kuwa inaweza kutoa mchango mkubwa katika nyanja za tiba na afya, usalama wa chakula, teknolojia za viwandani, na kuhakikisha mustakabali wa nishati endelevu kwa vizazi vijavyo.

Silaha za nyuklia hazileti usalama

Alisisitiza kuwa Iran haitakubali kamwe hali ambapo elimu na teknolojia ya nyuklia inageuzwa kuwa haki ya kipekee ya nchi chache tu duniani. Rais aliongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haichukulii silaha za nyuklia kama chanzo cha kuleta usalama.

Pezeshkian alisema kuwa kadhia ya nyuklia haiwezi kupatiwa ufumbuzi katika medani za vita, na akabainisha kuwa suluhu pekee ni kufikiwa kwa makubaliano yatakayotoa uhakikisho thabiti na wa kuaminika kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu asili ya amani ya mpango wa Iran, huku yakilinda na kuhakikisha haki za kimsingi za taifa la Iran.

Aidha, Pezeshkian aliweka bayana ushirikiano wa kikanda kama nguzo nyingine muhimu ya sera ya usalama ya Iran. Alisisitiza kuwa Iran haizichukulii nchi jirani kama washindani katika masuala ya usalama, bali inatamani kuona majirani imara na wenye nguvu kwa ajili ya ustawi na utulivu wa eneo zima.

Kadhalika, alizungumzia suala la Lango-Bahari la Hormuz, akibainisha kuwa nchi hazipaswi kwa wakati mmoja kutafuta manufaa kutoka kwa njia hiyo muhimu ya maji huku zikimzuia mlinzi wake wa kihistoria, yaani Iran, kutekeleza haki yake ya uhuru wa urambazaji, ikiwemo katika maji yake mwenyewe.

Alikosoa vikali uwepo wa vikosi vya wanamaji vya adui katika eneo hilo na ubebaji wa silaha, mabomu, na makombora kupitia njia hiyo, akisema kuwa vitendo hivyo haviwezi kuleta usalama wa kudumu wa baharini. Alionya kuwa uhuru wa urambazaji na usalama wa nchi zinazopakana na bahari lazima vizingatiwe kwa pamoja.

Palestina ni jeraha linaloendelea

Akigeukia suala la Palestina, Rais Pezeshkian alieleza kuwa suala hilo ni “jeraha linaloendelea” katika dhamiri ya jumuiya ya kimataifa, na Gaza imekuwa mfano wa kushindwa kwa mifumo ya kimataifa kuzuia mateso ya raia.

Alibainisha kuwa zaidi ya watu 80,000 wameuawa Gaza akielezea hali hiyo kuwa ni mauaji ya kimbari. Alisisitiza kuwa amani ya kudumu katika Asia ya Magharibi haiwezekani bila kuwepo kwa haki kamili kwa Wapalestina.

Rais Pezeshkian alisema kuwa mapambano (Muqawama) yataendelea maadamu uvamizi, uchokozi, na dhulma vitaendelea kuwepo. Alibainisha kuwa ushambuliaji wa mabomu, mzingiro, na kufukuzwa makazi kwa nguvu haviwezi kuwalazimisha watu kusalimu amri wala kuacha mapambano yao.

Aidha, alisema kuwa masuala ya kikanda yanapaswa kutatuliwa na nchi za eneo hili badala ya kuwa kisingizio cha vita vinavyohusisha madola ya mbali. Alieleza kuwa uhuru wa kistratijia unamaanisha kuwa uhusiano na madola ya nje haupaswi kugeuzwa kuwa nyenzo za kuanzisha vita dhidi ya nchi jirani.

Iran haijawahi kuanzisha vita

Pezeshkian alisisitiza kuwa Iran haijawahi kuwa muanzishaji vita na mara kadhaa imedhihirisha utayari wake wa kufanya mazungumzo. Alisema kuwa vita vimekuwa vikilazimishwa dhidi ya Iran, lakini nchi imethibitisha kuwa itajihami vilivyo na haitaviogopa vita pindi inapolinda mamlaka na ardhi yake.

Wakati huo huo, alieleza kuwa Iran haikwepi mazungumzo katika kutafuta amani. Alibainisha kuwa mashauriano na ulinzi ni nguzo mbili zinazokamilishana, akisema Iran iko tayari kwa mazungumzo ya maana, lakini inakataa katakata kuburuzwa au kukubali lugha ya vitisho na kulazimishwa mambo.

Pezeshkian alitenga sehemu ya hotuba yake kukemea undumakuwili (vipimo viwili) unaotawala mfumo wa kimataifa. Alilinganisha jinsi shughuli za nyuklia za amani za Iran zinavyochunguzwa kwa masharti magumu, huku utawala ghasibu wa Kizayuni ukiachwa ukiwa na mamia ya vichwa vya silaha za nyuklia bila hata kuwa mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Haki sawa kwa nchi zote

Alisisitiza kuwa sheria za kimataifa na haki za binadamu hazipaswi kutekelezwa kulingana na maslahi na matakwa ya madola yenye nguvu pekee. Alionya kuwa vikwazo vya kidhalimu vya kiuchumi na hatua zingine za upande mmoja huishia kuwaumiza moja kwa moja watu maskini, wagonjwa, na raia wengine wasio na hatia.

“Haki za binadamu si nyenzo ya ushindani wa kijiografia na kisiasa,” alisema Rais, akitoa wito wa kuwepo kwa haki sawa na wajibu sawa kwa nchi zote.

Alitoa indhari kwamba iwapo sheria za kimataifa zitatekelezwa pale tu zinaponufaisha nchi zenye nguvu, mataifa mengi zaidi yatafikia uamuzi kuwa lazima yategemee nguvu zao wenyewe pekee ili kuhakikisha usalama wao, jambo litakaloifanya dunia kuwa mahali hatari zaidi kuishi.

Pezeshkian alisisitiza kuwa mfumo wa kimataifa haupaswi kurudi nyuma na kutawaliwa na sheria ya msituni na nguvu za kidikteta. Alibainisha kuwa nguvu za kijeshi hazipaswi kuchukua nafasi ya uhalali wa kisheria; vikwazo havipaswi kuchukua nafasi ya diplomasia; mauaji ya kigaidi hayapaswi kuchukua nafasi ya siasa; na vita havipaswi kamwe kuchukua nafasi ya mazungumzo.

Iran inataka ushirikiano na amani

Alieleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inanyoosha mkono wa ushirikiano kwa ulimwengu na kutoa wito wa amani na uadilifu kutokana na nafasi ya nguvu na kujiamini, na si kutokana na udhaifu. Aliongeza kuwa nchi za eneo hili ama zitajenga usalama wa pamoja kwa ushirikiano, au zote zitateseka kwa pamoja chini ya kivuli cha ukosefu wa amani.

Kadhalika, alitoa wito wa kuwepo kwa mfumo mpya wa kimataifa uliojengwa juu ya misingi ya usawa baina ya mataifa, uadilifu, haki, na utashi wa pamoja wa wanadamu wote, akisisitiza kuwa amani na uadilifu lazima vitumike kwa wote bila ubaguzi.

Mantiki ya Kibabe

Katika kuhitimisha hotuba yake, Pezeshkian alikosoa vikali kauli zilizotolewa siku moja kabla na rais wa Marekani, akizieleza kuwa ziliakisi mantiki ya kibabe na kulazimisha mambo, na kwamba zinakinzana waziwazi na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Alisisitiza kuwa vitisho na mashinikizo havitawavunja moyo wananchi wa Iran, bali vitazidi kuwaunganisha na kuimarisha azma yao thabiti ya kusimama imara. Sambamba na hilo, alithibitisha tena utayari wa Iran kwa mazungumzo ya kiheshima, huku akiweka bayana kuwa Tehran haitakubali wala kusalimu amri mbele ya lugha ya mabavu.

Alihitimisha kwa kuitaka dunia itambue kuwa Iran haitapiga magoti mbele ya vitisho vyovyote vile, na itaendelea kutetea kwa dhati uhuru na mamlaka yake kamili, huku ikipigania mustakabali uliojengwa juu ya usalama, uadilifu, heshima, na haki sawa kwa mataifa yote duniani.

3499146

Habari zinazohusiana
captcha