IQNA

16:32 - September 26, 2026
Habari ID: 3482821

Malaysia yatoa wito wa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza 'Uchumi wa Halal'

IQNA – Malaysia imetoa wito kwa nchi mbalimbali duniani kushirikiana kwa karibu ili kukuza uchumi wa halal duniani.

w

Siku ya Ijumaa, Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia, Ahmad Zahid Hamidi, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kupanua wigo wa uchumi wa halal ulimwenguni.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Halal ya Malaysia (MIHAS 2026) na Mkutano wa Kimataifa wa Halal (GHaS 2026) uliofanyika katika Kituo cha Biashara na Maonyesho ya Kimataifa cha Malaysia (MITEC), alitoa wito kwa watunga sera na wafanyabiashara kutumia fursa za mahitaji yanayokua ya sekta hiyo ili kuzalisha fursa za kibiashara zenye matokeo. Hafla hiyo iliwakutanisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali, maafisa wa serikali, na wawakilishi wa sekta ya viwanda kutoka pande zote za dunia.

‘Geuzeni Malengo Kuwa Biashara na Ajira’

Zahid alibainisha kuwa ni asilimia 14.7 pekee ya kampuni zilizothibitishwa kuwa za 'Halal' nchini Malaysia ndizo zinazojihusisha na mauzo ya nje, akisisitiza hitaji la kuzisaidia kampuni nyingi zaidi ziweze kushindana katika soko la kimataifa. “Uthibitisho (vyeti vya halal) ni mwanzo tu wa safari hiyo,” alisema. “Ili kufikia malengo yetu, ni lazima tuzisaidie kampuni hizi nyingi zaidi kushindana katika masoko ya ng’ambo.”

Naibu Waziri Mkuu alielezea mafanikio ya hivi karibuni ya kibiashara ya Malaysia, akibainisha kuwa maonyesho ya MIHAS yaliyofanyika Dubai na Shanghai yaliingiza mauzo ya Ringgit bilioni 2.2 (dola za Marekani milioni 540) na Ringgit bilioni 3.2 (dola za Marekani milioni 785) mtawalia. “Na tujenge azma yetu ya pamoja kuwa fursa za kibiashara, uwekezaji, na ajira,” alisema Zahid. “Kazi yetu lazima iendelee zaidi ya mkutano huu. Mafanikio yatapimwa kwa vizuizi tunavyoondoa, ushirikiano wa kudumu tunaoujenga, na wafanyabiashara wanaofikia masoko mapya.”

Kujenga Imani Kupitia Mfumo Bora

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia anayeshughulikia Masuala ya Kidini, Zulkifli Hasan, alisema kuwa maendeleo ya sekta ya halal yanategemea misingi ya Sharia, mfumo bora, na maadili ili kuimarisha imani. “Halal si suala tu la viwango, uthibitisho, au biashara pekee,” alisisitiza. Zulkifli aliongeza kuwa Mfumo wa Uthibitisho wa Halal wa Malaysia wa JAKIM unajenga “mnyororo wa imani” unaoimarisha matumaini ya kimataifa katika bidhaa za halal.

Zulkifli alibainisha kuwa Malaysia inasalia na dhamira ya kupanua wajibu wake kupitia uvumbuzi, teknolojia, na ushirikiano wa kimkakati. Mkutano wa GHaS 2026 unafanyika chini ya kaulimbiu “Sharia na Uadilifu: Kuwezesha Mfumo wa Kiuchumi wa Halal Duniani,” huku maonyesho ya MIHAS 2026 yakiendelea hadi Septemba 26 katika kituo cha MITEC chini ya kaulimbiu “Kujenga Imani, Kuimarisha Ustahimilivu,” yakikutanisha wawakilishi wa sekta hiyo duniani kote.

Inafaa kuashiria hapa kuwa neno Halal ni Kiarabu chenye maana ya "kuruhusiwa" au "halali". Katika mafundisho ya Kiislamu, halal inajumuisha vyote viwili: bidhaa na huduma. Kila kitu kinachoruhusiwa na dini hutambulika kama halal, wakati kinyume chake huitwa haram (kilichokatazwa). 

3499161

 

Habari zinazohusiana
captcha