IQNA – Meya wa Jiji la New York amemtaja waziri mkuu wa utawala wa Israel kama “mbunifu mkuu wa mauaji ya kimbari ya kutisha.”
Zohran Mamdani amerejelea upya ukosoaji wake dhidi ya Benjamin Netanyahu, akitoa wito kwa Marekani kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kutekeleza vibali vyake vya kukamatwa, kikiwemo kibali kinachomkabili Netanyahu.
Mamdani alitoa kauli hizo wakati wa mahojiano na mchekeshaji na mwandaaji wa podikasti, Theo Von, katika kipindi cha This Past Weekend, siku chache baada ya Netanyahu kumkosoa meya huyo wa New York wakati wa hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
“Kama ingekuwa uamuzi wangu, serikali ya Marekani ingekuwa imejiunga na ICC na kuheshimu kila kibali kimoja kilichotolewa nao,” alisema Mamdani.
Akimgusia Netanyahu, aliongeza: “Unapouliza kuhusu waziri mkuu (wa Israel), tunazungumza kuhusu mbunifu mkuu wa mauaji ya kimbari ya kutisha.”
Mahakama ya ICC ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Netanyahu mnamo Novemba 2024 kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu zinazohusiana na vita vya maangamizi vya Israel katika Ukanda wa Gaza. Israel na Marekani si wanachama wa ICC na zimekataa mamlaka ya mahakama hiyo katika kadhia hiyo.
Katika podikasti hiyo, Von alimuuliza Mamdani ikiwa aliamini kuwa Netanyahu alipaswa kukamatwa alipokuwa New York. Mamdani alisema msimamo wake wa awali ulibadilika baada ya kuchunguza mamlaka ya kisheria aliyonayo meya wa New York.
“Kama serikali ya shirikisho ingejiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ingeweza kutekeleza kibali cha kumkamata,” alisema.
Wakati Von alipobainisha kuwa Marekani si mwanachama wa mahakama hiyo, Mamdani alijibu: “Sisi si wanachama. Lakini ninaamini tunapaswa kujiunga nayo, na kwamba tunapaswa kutekeleza vibali vyake.”
Alisema suala hilo halimhusu Netanyahu pekee, bali linahusu kuaminika kwa sheria za kimataifa.
“Kadiri watu wanavyoona mtu akikiuka sheria au kanuni na kusiwe na uwajibikaji wowote, ndivyo wanavyozidi kuanza kujiuliza ikiwa kanuni hizo zina thamani yoyote,” alisema Mamdani.
3499256