IQNA— Mufti wa Uganda, Sheikh Shaban Ramadhan Mubaje, amezindua kamati maalum ya watu saba yenye jukumu la kutarjumu na kutafsiri Qur’ani Tukufu katika lugha ya Kilangi (Lango), ambayo ni lugha ya Kiniloti inayozungumzwa katika eneo la Lango, kaskazini mwa Uganda.
Hatua hii ya kutafsiri Kitabu Kitukufu katika lugha ya Kilangi inalenga kuyafanya mafundisho ya Kiislamu yaweze kufikika kwa urahisi zaidi kwa Waislamu wanaozungumza lugha hiyo kaskazini mwa Uganda. Kamati hiyo ilizinduliwa jijini Lira wakati wa sherehe za maadhimisho ya Maulidi au kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Kamati hiyo imewakutanisha wanazuoni wa Kiislamu, walimu wa elimu ya dini, na wataalamu wa lugha, ambao watafanya kazi ya kutafsiri Qur’ani katika lugha hiyo inayozungumzwa sana katika ukanda wa Lango. Juhudi hizi zina lengo la kuwawezesha Waislamu wanaozungumza Kilangi kuelewa vyema mafundisho na ujumbe wa Qur’ani Tukufu kwa lugha ambayo ni rahisi kwao kuielewa.
Mradi huu umefadhiliwa kifedha na Haj Masoud Obeid, mfanyabiashara mwenye makazi yake jijini Kampala, ambaye ana asili ya eneo la Lango. Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Mufti Ramadhan Mubaje alimsifu Haj Obeid kwa kuunga mkono mpango huu na akawahimiza Waislamu wengine kujitokeza kusaidia programu zinazolenga kuimarisha elimu ya Kiislamu na kuustawisha umma wa Kiislamu kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Mufti Ramadhan Mubaje pia alitangaza mipango yake ya kurejea eneo la Lango kwa ajili ya ziara ya wiki nzima ya mazungumzo na viongozi wa Kiislamu pamoja na wadau wengine, kufuatia wasiwasi uliopo kuhusu masuala ya uongozi na usimamizi wa mali za Waislamu mkoani humo. Alisema ziara yake itampa fursa ya kukutana na wadau mbalimbali ili kutafuta suluhu za kudumu kwa changamoto zinazoukabili umma wa Kiislamu katika eneo hilo.
Vilevile, Mufti Ramadhan Mubaje aliwahimiza Waislamu kudumisha mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) kuhusu udugu, heshima, na kuishi kwa amani, akisisitiza kuwa maadili haya yanaendelea kuwa muhimu kwa ustawi wa jamii ya Kiislamu. Sherehe hizo za Maulid ya Mtume Muhammad (SAW) zilihitimishwa kwa hafla ya shukrani iliyoandaliwa na wanawake wa Kiislamu wa Lango, wakiongozwa na mwakilishi wao wa kitaifa.
3499294