IQNA— Mkuu wa Makao Makuu ya Kitaifa ya Quds na Intifada nchini Iran amesema kuwa Operesheni ya “Kimbunga cha Al-Aqsa” (Tufan Al Aqsa), iliyotekelezwa na vikosi vya mapambano vya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023, imeifanya kadhia ya Palestina kuwa suala kuu na la kipaumbele katika ajenda za dunia nzima.
Akielezea Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa kama nukta ya mageuzi katika mapambano ya watu wa Palestina, Ramazan Sharif alibainisha kuwa operesheni hiyo ilivunja dhana potofu ya “kutoshindika” kwa utawala wa Kizayuni, na kwa mara nyingine ikalirejesha suala la Palestina, ambalo Wazayuni walijaribu kulifuta na kulisahau, kuwa ajenda muhimu zaidi duniani.
Alitoa kauli hizo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Tehran siku ya Jumanne, kuadhimisha kumbukumbu ya operesheni hiyo.
“Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilikuwa ni operesheni ya kijeshi. Ingawa mapambano ya watu wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni yameendelea kwa zaidi ya miongo saba, operesheni hii iliandaliwa na kutekelezwa katika kipindi ambacho Wazayuni walikuwa wakidai kuwa suala la Palestina ni kama ukurasa uliokwisha kufungwa,” alisema.
“Walidai kuwa wamejenga ngome imara na ngome isiyopenyeka, wakijigamba kuwa hakuna yeyote mwenye uwezo wa kuwakabili. Walipoulizwa kuhusu msingi wa madai hayo, walikuwa wakitolea mfano vita walivyopigana dhidi ya mataifa ya Kiarabu, hususan kushindwa kwa mataifa kadhaa ya Kiarabu kwa wakati mmoja. wakisema hakuna yeyote mwenye uwezo wa kuwathubutu. Walisema haya kwa uwazi kabisa, wakiamini kuwa suala la Palestina lilikuwa limeshamalizika.”
Afisa huyo aliongeza kuwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilionyesha tena kwa dunia roho ya kudumu ya mapambano na Jihad, pamoja na uhai wa kadhia ya Palestina, huku ikiuacha utawala wa Kizayuni katika hali ngumu na ya hatari.
Akibainisha kuwa miaka mitatu imepita tangu kuzinduliwa kwa operesheni hiyo, alisema kuwa hili si suala la mjadala wa kawaida tu. “Kila operesheni ya kijeshi inahusisha mipango, malengo, ratiba ya utekelezaji, na matokeo. Kuhusu mafanikio ya operesheni hii, lazima isemwe kuwa Kimbunga cha Al-Aqsa kilikuwa operesheni yenye mafanikio makubwa na hatua muhimu ya mabadiliko katika mapambano ya watu wa Palestina.”
Sharif aliendelea kusema, “Leo, katika maadhimisho ya tatu ya operesheni hiyo, tunaona kuwa Kimbunga cha Al-Aqsa kimeweka utawala wa Kizayuni katika mkwamo mkubwa. Zaidi ya makazi 50 ya Wazayuni yalitekwa au kutishiwa kutekwa wakati wa operesheni hiyo, ukweli ambao uliharibu dhana ya uwezo wa Israel wa kutoshindika.”
Akirejelea mifumo ya kiusalama na ulinzi ya utawala wa Kizayuni, alisema, “Wazayuni walikuwa wakizungumzia ‘Ukuta wa Chuma’ (Iron Wall) na vizuizi vya tabaka saba, wakidai kuwa wangeweza kuhisi na kulenga hata mchwa mmoja anayepita eneo hilo. Lakini Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilivunja hadithi hiyo, ikionyesha kuwa kama nia ipo, na kwa hakika ipo miongoni mwa watu wa Palestina katika hali yake bora na ya juu kabisa, inawezekana kusimama imara dhidi ya utawala huu.”
3499299