IQNA

19:43 - October 07, 2026
Habari ID: 3482872

Hamas yapongeza Kimbunga cha Al-Aqsa kama ‘Nukta ya Mageuzi ya Kihistoria’ katika Mapambano ya Palestina

IQNA — Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa siku ya Jumatano kuadhimisha kumbukumbu ya miaka mitatu tangu kuzinduliwa kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa (Tufan Al-Aqsa).

o

Harakati hiyo imeelezea operesheni hiyo ya tarehe 7 Oktoba 2023 kama “nukta ya mageuzi ya kihistoria” katika mapambano ya Wapalestina, na kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya uvamizi ni haki halali ya kumaliza ukaliaji mabavu na kukomboa ardhi na maeneo matakatifu.

Katika taarifa yake, Hamas ilisema kuwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilileta sauti ya watu wateule na wanyonge wa Palestina kwenye hadhara ya dunia baada ya miongo kadhaa ya kusahaulika na kupuuzwa huku kukiwa na uungwaji mkono wa sera za Israel.

Harakati hiyo ilipongeza msimamo thabiti na uvumilivu wa Wapalestina huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Quds Tukufu (Jerusalem), ikisisitiza kuwa licha ya vita vya uharibifu, Wapalestina wanaendelea kupigania ukombozi wa ardhi yao.

Hamas ilielezea kurejea kwa Wapalestina katika makazi yao na maeneo yaliyoharibiwa kama ishara ya kukataa kwao mipango ya kuwahamisha kwa nguvu na kufuta asili yao (ethnic cleansing).

Pia, Hamas ilielezea operesheni hiyo ya Oktoba 7 kama jibu la miongo kadhaa ya mzingiro, mashambulizi ya kijeshi, mauaji, na unyang’anyi wa haki za Wapalestina, ikisisitiza kuwa mzozo huo ulianza kabla ya Oktoba 7 na bado haujaisha.

Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, Hamas ilisema kuwa Israel imetenda mauaji ya kimbari na kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia, ikibainisha kuwa zaidi ya Wapalestina 74,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 175,000 wamejeruhiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Harakati hiyo pia ilirejelea maelfu ya Wapalestina waliotoweka na kuzuiliwa gerezani, ikisisitiza kuwa vitendo hivi ni jinai zilizothibitishwa ambazo hazitafutika kwa muda kupita (statute of limitations).

Hamas iliongeza kuwa “vita vya maangamizi” dhidi ya Wapalestina havijasimama licha ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ikimtuhumu Israel kwa kuendeleza kile ilichokiita “mauaji ya kimya kimya” kupitia mashambulizi yanayoendelea, mzingiro, na vizuizi vya upatikanaji wa mahitaji ya msingi.

Harakati hiyo ilisema kuwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaanze kutekezwa, Wapalestina wapatao 1,500 wameuawa shahidi na zaidi ya 5,000 wamejeruhiwa.

Hamas pia ilitaja kuendelea kwa operesheni za kijeshi za Israel, ukamataji, na ubomoaji wa nyumba huko Jerusalem na Ukingo wa Magharibi, pamoja na ongezeko la mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina, mali zao, na ardhi yao.

Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, Hamas ilisema kuwa vitendo vya Israel vimesababisha kupungua kwa uungwaji mkono wa kimataifa kwa nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na miongoni mwa washirika wake wa jadi wa Magharibi.

Harakati hiyo ilielezea kujiondoa kwa baadhi ya wajumbe katika mikutano ya Umoja wa Mataifa kama ishara ya kutengwa kisiasa kwa Israel kunakozidi kuongezeka.

Aidha, Hamas ilisema itaendelea na juhudi za kuanzisha “mkakati thabiti wa kitaifa na wa mapambano” unaowahusisha makundi na mirengo mbalimbali ya Palestina, ikiuelezea kama njia ya kukabiliana na sera za Israel.

Harakati hiyo ilikaribisha kampeni zinazozidi kukua duniani kote za kususia na kuweka vikwazo dhidi ya Israel na taasisi zake za kitaaluma, kiuchumi, na kiusalama, na ikatoa wito kwa wanaharakati na wafuasi wa Palestina duniani kote kuongeza nguvu katika juhudi hizo.

Katika sehemu ya mwisho ya taarifa hiyo, Hamas na makundi mengine ya mapambano ya Palestina yamethibitisha tena utayari wao katika wajibu wao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, na kusema yatafanya kazi na wapatanishi kuhakikisha mafanikio yake.

Hamas pia iliwajibisha Marekani na wapatanishi wanaosimamia makubaliano hayo kuhakikisha kuwa Israel inatekeleza ahadi zake, na ikatoa wito wa kutekelezwa kwa ramani ya barabara iliyokubaliwa, ambayo inapaswa kuleta mwisho kamili wa mashambulizi, uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina, ujenzi mpya wa Gaza, na kuondoka kabisa kwa vikosi vya wavamizi kutoka Ukanda wa Gaza.

3499313

Habari zinazohusiana
captcha