IQNA— Naibu Waziri wa Utamaduni wa Iran amesema kuwa Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Tehran yanapaswa kupelekea wageni na watazamaji kujenga uhusiano wa kina zaidi na Kitabu Kitukufu cha Qur’ani.
Hujjatul Islam Hamidreza Arbab Soleimani, ambaye pia anaongoza Kituo Kikuu cha Qur’ani na Etrat katika Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu Iran, alitoa kauli hizo katika kikao kilichofanyika mjini Tehran siku ya Jumanne.
Kikao hicho kilifanyika kwa ajili ya kujadili maandalizi ya Toleo la 34 la Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu, ambalo linatambulika kama moja ya matukio makuu na ya kihistoria ya Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu.
Alisema kuwa neno “kimataifa” lililopo kwenye jina la maonesho haya linaweka jukumu na mzigo mkubwa kwa mabega ya waandaaji.
Alieleza kuwa maonesho haya ni jukwaa la kuwasilisha kazi mpya za Qur’ani za nchi na kutangaza kazi mashuhuri kutoka ulimwengu wa Kiislamu; kwa hiyo, kuwasilisha bidhaa yoyote isiyo na kiwango kinachotakiwa kunachukuliwa kuwa ni kushindwa kutekeleza lengo kuu.
Akielezea malengo ya mwisho ya maonesho hayo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na ujuzi na kuelekeza fikra kwenye Qur’ani. “Lengo letu kuu linapaswa kuwa ni maonesho haya kuleta ongezeko la imani na uhusiano wa kina kati ya wageni na aya za Mwenyezi Mungu, na kufikia lengo hili kunahitaji mtazamo sahihi na mipango makini.”
Kiongozi huyo wa kidini alisisitiza haja ya kuwepo kwa utaalamu, moyo wa kujitolea, uzoefu, na mtazamo wa kihalisia katika kufanya maamuzi ya kuandaa Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani.
Pia alitoa wito wa kuanza kwa wakati kwa shughuli za kamati ya maudhui ili iweze kupitia kwa makini na kujibu mapendekezo yote yanayohusu toleo la 34 la maonesho hayo.
Akirejelea hali ya sasa ya nchi, Hujjatul Islam Arbab Soleimani alisisitiza ulazima wa kupanga mikakati kwa werevu katika sekta ya kimataifa, akibainisha kuwa sekta ya habari na vyombo vya habari ina nafasi ya pekee katika hafla hii, na kuanzishwa kwa kikundi kazi maalum cha vyombo vya habari kutaimarisha zaidi sekta hiyo.
Aidha, alipendekeza kutumia uzoefu wa nchi mbalimbali za Kiislamu katika kuandaa maonesho ya Qur’ani na akatoa wito wa kuboresha misingi ya kiutendaji.
Hatimaye, afisa huyo alipendekeza kuwa maonesho ya Qur’ani ya mtandaoni yaandaliwe na kutekelezwa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika mazingira maalum, ili uwezo mkubwa uliopo kwenye mtandao utumike kikamilifu kutimiza malengo ya maonesho hayo.
3499312