IQNA — Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, amesisitiza kuwa programu zinazohusu Qur’ani hazipaswi kuishia tu kwenye usomaji wa sauti na kuhifadhi (hifdhi), bali lazima ziwe na lengo la kuwakaribisha Waislamu zaidi na zaidi na Kitabu Kitukufu kupitia kusoma, kusoma kwa kina (kudarisi na kutafakari maana za aya), kufahamu, kuhifadhi, kutekeleza, na kuzingatia mafundisho yake maishani.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook siku ya Jumanne huku Mashindano ya 66 ya Kimataifa ya Qur’ani ya Malaysia yakiwa yanaendelea, Waziri Mkuu Anwar alisisitiza kuwa Waislamu lazima wakumbatie nyanja mpya za maarifa, zikiwemo akili mnemba (Artificial Intelligence - AI), kompyuta za quantum, na mifumo ya kidijitali, huku wakibaki wameshikilia imani thabiti, maadili, na misingi ya Kiislamu.
Alisema marekebisho ya jamii ya Waislamu (Islah) lazima yaende zaidi ya kuhudhuria mikusanyiko ya kidini, na yatafsiriwe katika kutafuta maarifa, ujenzi wa tabia njema, na uwajibikaji. Katika ujumbe wake, aliandika: “Kwa hivyo, juhudi za marekebisho lazima ziende zaidi ya kuhudhuria makongamano kama haya kwa kuthamini hekima ya Qur’ani, huku tukiwa na ujasiri wa kumudu nyanja mpya za maarifa, ikiwemo akili mnemba, zilizojikita katika imani thabiti na tabia tukufu.”
Anwar alionya kuwa kumudu AI na teknolojia nyingine zinazoibukia si jambo la hiari bali ni dharura, akionya kuwa jamii ya Waislamu itakayopuuza nyanja hizi za maarifa itajikuta ikichelewa kimaendeleo. “Changamoto ni jinsi tunavyotumia maarifa na teknolojia mpya kama vile kompyuta za quantum, akili mnemba, na kidijitali, huku tukibaki tumeshikamana na imani, maadili na tabia zetu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alionya kuwa harakati za maendeleo ya kiteknolojia na maarifa mapya zisije zikafanyika kwa gharama ya kuacha imani na maadili. “Maadili yetu lazima yatetewe. Hatupaswi kuruhusu hamu yetu ya mabadiliko au utafutaji wa maarifa mapya kutusababisha tuache misingi ya imani na maadili, au kuruhusu tabia zetu kama Waislamu wema kupuuzwa.”
Kuhusu utangazaji wa Uislamu (Da’wah), Anwar alisisitiza kuwa lazima uendeshwe kwa roho ya huruma na upendo, badala ya hamu ya kuonyesha ubora wa kiakili au maarifa. Alisema roho ya huruma inapaswa kuonekana kupitia mbinu ya kiungwana, ikiwa ni pamoja na utayari wa kujadiliana, kusikiliza maoni tofauti, na kufikia muafaka.
Katika kurejea historia, Anwar aligusia swali lililoulizwa na msomi wa Sambas, Sheikh Muhammad Basyuni Imran kwa Sayyid Rashid Rida mwaka 1929 kuhusu sababu za kudorora kwa Waislamu, swali ambalo lilijibiwa na Amir Shakib Arsalan mwaka 1930. Alisema swali hilo bado ni muhimu leo, kwani mwamko wa Waislamu unahitaji upya katika maarifa na mwenendo, pamoja na uelewa wa kina wa dini unaotafsiriwa katika vitendo na uwajibikaji.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kusema kuwa Malaysia inalenga kuzalisha “Kizazi cha Qur’ani” ambacho nyoyo zao zimeunganishwa na Mwenyezi Mungu, zinazotafuta maarifa kwa bidii, na zinazoleta huruma katika shughuli zao zote. “Hiki ndicho kizazi cha kipekee cha Qur’ani tunachotaka kuzalisha, kile ambacho moyo wake umeunganishwa na Mungu, kinachotafuta maarifa kwa bidii na kinacholeta huruma katika utangazaji wake.”
Alimalizia kwa kunukuu aya ya 159 ya Surah Al-Imran, inayosisitiza upole, msamaha, na kushauriana katika kushughulikia mambo ya maisha.
3499309