IQNA

18:56 - November 01, 2026
Habari ID: 3482981

Trump awahimiza wapiga kura kumrudisha “Kwao” mgombea Muislamu aliyezaliwa Marekani

IQNA – Mgombea Muislamu wa kiti cha Seneti, aliyezaliwa na kukulia Marekani, ameambiwa na Donald Trump “arudi alikotoka,” kauli iliyozua lawama.

Abdul El-Sayed
 

Katika mkutano wa kampeni huko Florida usiku wa Ijumaa, rais huyo wa Marekani alirudia mashambulizi yake dhidi ya Abdul El-Sayed, mgombea wa chama cha Democratic katika kinyang’anyiro cha Seneti cha jimbo la Michigan.

Trump alidai mbele ya wafuasi wake kuwa eti “Abdul si mpenzi mkubwa wa Wayahudi, na si mpenzi mkubwa wa watu weusi. Na natumaini mtampigia kura ya kupinga na kumrudisha alikotoka."

El-Sayed amemshutumu Trump kwa kueneza uongo ili kuwapotosha wapigakura. Ingawa ameikosoa Israel, hajawadharau wapigakura Wayahudi wala wenye asili ya Afrika au weusi.

Katika mkutano wa hadhara jimboni kwake siku ya Jumatatu, El-Sayed aliwaambia wapigakura: “Jina langu na imani yangu si sababu ya ninyi kushindwa kumudu bei ya mafuta, si sababu ya kushindwa kumudu chakula, si sababu ya kushindwa kulipa kodi ya nyumba au rehani, wala si sababu ya kushindwa kumwona daktari.”

Warepublican wamekita hoja zao kwenye masuala ya uhamiaji na dini kama mada kuu za uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwaka huu, wakizitumia kuwashambulia wapinzani kama El-Sayed walio katika mrengo wa kushoto zaidi wa chama cha Democratic.

Katika kampeni, Trump ametaja mafanikio yake ya kupunguza uvukaji haramu wa mipaka, akidai kuwa Wademocrat hapo awali waliruhusu wahamiaji “kumiminika katika mipaka yetu” na kwamba “wakishinda katika uchaguzi wa katikati ya muhula, watafanya hivyo tena.”

Kwa upande wao, wagombea wa Democratic wamemtuhumu rais kwa kutumia masuala hayo kugeuza fikira za watu kutoka kwa vita dhidi ya Iran na kupanda kwa bei kunakowaathiri Wamarekani wa kawaida kutokana na vita hivyo.

Gharama za maisha ndiyo kipaumbele cha wapigakura

Kura za maoni zinaonyesha kuwa wapigakura wa Marekani kutoka pande zote za kisiasa wanaipa kipaumbele shida ya gharama za maisha kuliko kukabili uhamiaji.

Zaidi ya theluthi mbili, yaani asilimia 69, ya wapigakura waliohojiwa na PF Global walisema wanataka wanasiasa wajikite kupunguza bei, huku asilimia 19 wakisema wapewe kipaumbele kuzuia uhamiaji haramu kuingia Marekani.

Utafiti huo wa Wamarekani 2,043, uliofanyika kati ya tarehe 28 na 30 Oktoba, ulibaini kuwa asilimia 89 ya Wademocrat wanaona gharama za maisha ndilo suala kubwa zaidi kwa uchaguzi wa katikati ya muhula wa tarehe 3 Novemba, huku asilimia 53 ya Warepublican wakisema vivyo hivyo.

Wamarekani wamebanwa na mgogoro wa mafuta duniani, uliozidishwa na vita haramu vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambavyo vimepandisha bei ya mafuta, chakula na bidhaa nyinginezo.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa Wamarekani wanaamini Uingereza inashughulikia uhamiaji vizuri zaidi kuliko Marekani, ambapo asilimia 29 ya wapigakura walisema Uingereza ina mkabala bora, ikilinganishwa na asilimia 19 waliosema kinyume chake.

Hata hivyo, uungwaji mkono wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) bado ni imara katika pande zote za vyama, huku wapigakura wengi wakisema bado wanaunga mkono taasisi hiyo licha ya shutuma kwamba imekuwa ya mkono mzito kupita kiasi.

Kwa jumla, asilimia 58 ya Wamarekani waliohojiwa na PF Global kabla ya uchaguzi huo walisema wanaunga mkono ICE na wanaamini misako yake imewazuia watu kuja Marekani. Hii ilijumuisha asilimia 59 ya waliompigia kura Kamala Harris katika uchaguzi uliopita wa urais, na asilimia 72 ya waliomchagua Trump.

Rais huyo amekuwa akiwaambia wapigakura mara kwa mara wajifanye yeye yumo kwenye karatasi ya kura katika uchaguzi huo wa katikati ya muhula, huku hofu ikiongezeka kuhusu idadi ndogo ya wapigakura katika kinyang’anyiro hiki muhimu cha kuwania Bunge la Congress.

Chama cha Democratic kinatarajiwa kwa kiasi kikubwa kutwaa udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, na kuna uwezekano mdogo kwamba kinaweza kurejesha Seneti. Hilo lingeminya vikali madaraka ya kisiasa ya Trump kwa kipindi kilichosalia cha urais wake.

Wademocrat wanahitaji kupata viti vinne vya ziada ili kushinda Seneti, na kinyang’anyiro cha Michigan kinatarajiwa kuwa mojawapo ya medani kuu za mapambano.

Kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha El-Sayed yuko mbele kidogo ya mpinzani wake wa Republican, Mike Rogers, katika jimbo hilo lenye mwelekeo usio dhahiri. Hata hivyo, kuna wasiwasi ndani ya chama cha Democratic kwamba mgombea wao ana misimamo ya mrengo wa kushoto kupita kiasi kuweza kuwavutia sehemu kubwa ya wakazi wa Michigan.

El-Sayed anataka kuifuta ICE kabisa, akisema misako yake ya uhamiaji inakiuka haki za kikatiba. Pia ameahidi kuongeza kodi kwa mabilionea na mashirika tajiri, na kusitisha msaada wote wa kijeshi wa Marekani kwa Israel.

Rogers ameahidi kupunguza kodi kwa familia zinazofanya kazi, na kuimarisha ulinzi wa mipaka na utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

3499621

 

Habari zinazohusiana
captcha