IQNA – Miongozo mipya dhidi ya chuki dhidi ya Wayahudi (anti-Semitism) iliyopitishwa na serikali ya Uingereza inaweza kubana uhuru wa kujieleza shuleni na kuwatia doa wanafunzi Waislamu.
Fatima Rajina, msomi bingwa wa masuala ya Waislamu wa Uingereza, rangi na utambulisho, anasema uamuzi wa serikali wa kuunganisha mijadala kuhusu Palestina na sera za ulinzi wa watoto pamoja na mpango wa kupambana na itikadi kali wa Prevent, unahatarisha kugeuza harakati za kuunga mkono Palestina kuwa suala la kiusalama.
Idara ya Elimu ya Uingereza imekubali mapendekezo yote 27 ya mapitio huru kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi katika shule na vyuo. Mapendekezo hayo yanajumuisha kuhimiza shule kupitisha ufafanuzi wa Muungano wa Kimataifa wa Kumbukumbu ya Mauaji ya Halaiki ya Wayahudi (IHRA) wa chuki dhidi ya Wayahudi, kuwazuia walimu kuvaa beji za kuunga mkono Palestina, na kujumuisha suala la chuki dhidi ya Wayahudi katika sera za ulinzi wa watoto shuleni.
Rajina anaonya kuwa kuhusisha chuki dhidi ya Wayahudi na mpango wa Prevent kunatia wasiwasi hasa, ikizingatiwa kuwa Waislamu wameathirika kwa kiwango kisicholingana na wengine katika rufaa za Prevent. Anasema mkabala huo mpya unahatarisha kuimarisha dhana kwamba wanafunzi Waislamu wanaohusika katika harakati za kuunga mkono Palestina ni vitisho vinavyowezekana kwa usalama.
Mwandishi huyo pia anahoji msimamo wa serikali kwamba shule hazipaswi kugeuka jukwaa la maandamano au kutoa kauli kuhusu matukio ya kisiasa ya kimataifa. Anakumbusha kuwa wanafunzi wa Uingereza wamemiminika mitaani na mitandaoni kwa miaka mitatu iliyopita kupinga uungaji mkono wa Uingereza kwa Israel katika vita vyake dhidi ya Gaza.
Zaidi ya hayo, anaangazia kile anachokiona kuwa ni unafiki au undumakuwili: wakati shule za Uingereza zimeshiriki katika shughuli za kuchangisha fedha kwa ajili ya Ukraine, mijadala kuhusu Palestina inazidi kuchukuliwa kama suala nyeti au hatari.
Rajina pia anaonya kuwa kupitisha ufafanuzi wa IHRA kunaweza kudhoofisha uhuru wa kitaaluma na kukatisha tamaa ukosoaji wa sera za serikali ya Israel. Ingawa ufafanuzi huo unasema kuwa kuikosoa Israel si chuki dhidi ya Wayahudi kwa asili yake, anasema utekelezaji wake kivitendo unaweza kutumiwa kunyamazisha mijadala halali.
Ripoti hiyo inahitimisha kuwa miongozo hiyo mipya inaweza kuzishawishi shule kuepuka kabisa kujadili Palestina, na hivyo kubana uhuru wa wanafunzi wa kufikiri na kujieleza, na kuimarisha ubaguzi dhidi ya Wapalestina, hasa dhidi ya wanafunzi Waislamu.
3499619