IQNA – Mwanazuoni mwandamizi wa Iran amelaani hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya Sheikh Hussein al-Ma’touq, mwanazuoni wa Kishia wa Kuwait, na kuzitaka mamlaka za nchi hiyo ya Kiarabu kuipitia upya hukumu hiyo mara moja.
Katika ujumbe wake, Mkurugenzi wa Hawza za Kiislamu Iran, Ayatullah Alireza Arafi, ameonya kuwa ubaguzi dhidi ya wanazuoni wa kidini unaweza kufungua mlango wa mipasuko na mifarakano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu.
Ayatullah Arafi alisema katika ujumbe wake: “Wakati ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto zisizo na kifani, zinazotokana na njama pana na zilizopangwa za maadui wa Uislamu, hasa utawala wa kiburi wa Marekani na utawala wa Kizayuni, habari za hukumu zisizo za haki na za kikatili zinazotolewa na mahakama za kanda hii zimeyauma sana mioyo ya Waislamu. Hilo ni kweli hasa kuhusu hukumu isiyo ya haki iliyotolewa na watawala wa Kuwait ya kumhukumu kifo Mujahid madhubuti, Hujjatul-Islam Sheikh Hussein al-Ma’touq, mwanazuoni mashuhuri na mtumishi mwaminifu wa wananchi wa Kuwait. Tukio hili limewasha wimbi la hasira na huzuni katika Ummah wote wa Kiislamu, pamoja na vituo vya elimu na hawza za Kiislamu nchini Iran na kote ulimwenguni.”
“Hatua hii, iliyotekelezwa kwa dharau dhahiri dhidi ya viwango vya kisheria na vya kibinadamu, na dhidi ya hadhi adhimu ya wanazuoni wa kidini, inavuka mipaka ya hukumu ya kimahakama tu. Ni shambulio dhidi ya utambulisho na haki za kidini za Waislamu na Mashia, na ni jaribio la wazi la kudhoofisha ushawishi na heshima ya wanazuoni wa Kiislamu.”
Kwa niaba ya hawza za Kiislamu, marajii wakuu wa taqlidi, wanazuoni wanaoheshimika na taasisi zinazohusiana, alilaani mwenendo huo wa dhulma na hukumu hiyo isiyo halali iliyotolewa.
“Ninaihimiza serikali na mamlaka husika za Kuwait, kwa kuongozwa na kanuni ya udugu wa Kiislamu, kuipitia upya hukumu hii mara moja, kulinda haki za msingi za wananchi Waislamu wenye heshima (hasa jamii ya Kishia ya Kuwait), na kuheshimu hadhi ya kielimu na kidini ya watu mashuhuri. Hatua hiyo ni ya lazima ili kuepusha maafa haya na kuzuia kupotoshwa kwa haki.”
Ayatullah Arafi aliongeza: “Ni muhimu pia kutambua kwamba ubaguzi wowote dhidi ya wanazuoni mashuhuri wa kidini haukiuki haki za mtu binafsi na za kijamii pekee, bali pia unahatarisha kuzaa mipasuko na mifarakano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. Hilo ndilo hasa wanalolitaka maadui wa Uislamu, na ni jambo ambalo serikali na wananchi wote wa Kiislamu wanapaswa kujitahidi kulikwepa.”
Alihitimisha kwa kumwomba Mwenyezi Mungu awaamshe watawala wa nchi za Kiislamu, na aupe ushindi Ummah wa Kiislamu dhidi ya maadui wake wa Kimarekani na Kizayuni.
3499631