IQNA – Mahakama moja ya Uswidi imemhukumu Jade Sandberg, mwenye itikadi kali ya mrengo wa kulia, kifungo cha nje na faini, kwa kosa la uhalifu wa chuki na kudharau Qur’ani Tukufu.
Hukumu hii inafuatia vitendo vyake dhidi ya Qur’ani Tukufu mjini Stockholm, mji mkuu wa Uswidi, mwaka 2024, kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Al-Quds al-Arabi.
Ijumaa jioni, Mahakama ya Wilaya ya Stockholm ilimhukumu Jade Sandberg, mwenye umri wa miaka 50, kifungo cha nje na faini ya krona 3,000 za Uswidi (takriban euro 275).
Mahakama pia iliamuru alipe krona 1,000 kwa mfuko wa waathiriwa wa uhalifu, na krona 17,000 (takriban euro 1,500) kwa serikali ili kugharamia ada ya wakili wake aliyeteuliwa na mahakama.
Hata hivyo, mahakama ilimwachilia huru Sandberg kwa shtaka jingine lililohusu kauli alizotoa wakati wa kitendo cha uchokozi nje ya msikiti mmoja mjini Stockholm, ambapo alisema: “Hatutaki Waislamu katika mitaa yetu.”
Tarehe 24 Agosti 2024, katika Uwanja wa Odenplan jijini humo, Sandberg alichoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu na kuipiga teke.
Alirusha tukio hilo moja kwa moja kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii, jambo lililopelekea kuwasilishwa kwa malalamiko rasmi dhidi yake. Aidha, Salwan Najm, mkazi wa Stockholm mzaliwa wa Iraq, pamoja na Jid Sandberg, walifanya maonyesho ya uchokozi huku wakiwa wamevaa mavazi ya kidini, kisha wakachoma nakala ya Qur’ani Tukufu mbele ya Bunge la Uswidi mjini Stockholm.
Video iliyotolewa inaonyesha watu hao wawili, wakiwa wameshika vipaza sauti, wakitoa kauli za chuki dhidi ya Uislamu na za kichochezi.
3499629