IQNA – Toleo la 27 la Mashindano ya Qur’ani Tukufu ya Sheikha Hind bint Maktoum limehitimishwa katika Falme za Kiarabu.
Toleo hili lilivutia washiriki 2,750, wanaume kwa wanawake, kutoka kote katika Umoja Falme za Kiarabu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 58 la ushiriki ikilinganishwa na toleo lililotangulia.
Mahudhurio hayo makubwa yanaonyesha kupanuka kwa wigo wa mashindano haya na hadhi yake miongoni mwa wanajamii wa rika mbalimbali.
Mashindano hayo huandaliwa na Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai, iliyo chini ya Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Kutoa Misaada mjini Dubai, kwa udhamini wa Sheikha Hind bint Maktoum bin Juma Al Maktoum.
Toleo la 27 lilirekodi ushiriki wa wanawake 1,357, sawa na asilimia 51.6, ikilinganishwa na wanaume 1,273, sawa na asilimia 48.4, hali inayoonyesha uwiano wa karibu katika ushiriki na fursa pana za ushindani. Raia wa Falme za Kiarabu ndio waliokuwa wengi zaidi kwenye orodha ya waliojisajili, wakiwa 1,944, sawa na asilimia 74 ya jumla, pamoja na wakazi wa mataifa mbalimbali wanaoishi nchini humo.
Ahmed Darwish Al Muhairi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Kutoa Misaada mjini Dubai na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai, alisema kuwa udhamini mkarimu wa Sheikha Hind bint Maktoum bin Juma Al Maktoum umeweka msingi wa safari endelevu ya Qur’ani, na kulifanya shindano hili kuwa tukio linalosubiriwa kwa hamu na familia za Kiemirati na zisizo za Kiemirati zinazotaka kushindana katika qiraa na kuhifadhi Qur’ani Tukufu.
Alibainisha kuwa ongezeko la ushiriki linaonyesha athari chanya ya udhamini huo na imani kubwa ya jamii ambayo shindano hili limejijengea kwa miaka mfululizo.
Al Muhairi alisema kuongezeka kwa ushiriki kunathibitisha thamani ya kuwekeza katika programu za Qur’ani kama njia ya kuwajenga watu binafsi, kuimarisha maadili na utambulisho, na kuimarisha mshikamano wa familia. “Hili linatutia moyo kujenga juu ya matokeo haya na kuliendeleza zaidi shindano hili kwa njia zinazokidhi mahitaji ya jamii.”
Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa familia, walimu, kamati za majaji na timu za maandalizi ambazo juhudi zao zilichangia mafanikio ya toleo hili, na kugeuza ushiriki kuwa safari ya kujifunza na ushindani chanya katika kutafuta kheri.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai aliongeza kuwa toleo la 27 limetoa viashiria muhimu vya maendeleo endelevu ya shindano hili, kwa kujenga juu ya mafanikio yake na kuboresha zaidi vipengele vyake mbalimbali. Alibainisha kuwa kiwango cha ushiriki wa Waemirati, pamoja na uwiano wa karibu kati ya ushiriki wa wanawake na wanaume, kinaonyesha mafanikio ya maboresho ya hivi karibuni yaliyoletwa katika matawi, makundi na vigezo vya shindano.
Kipengele cha kuhifadhi Juzuu Amma (sehemu ya 30 ya Qur’ani) kilirekodi usajili mwingi zaidi, kikiwa na washiriki 947, sawa na takriban asilimia 36 ya jumla, kikifuatiwa na kipengele cha kuhifadhi juzuu tatu chenye washiriki 367, na kipengele cha Sauti Bora chenye washiriki 357.
Kipengele cha kuhifadhi juzuu 20 kilivutia washiriki 289, huku 234 wakijisajili kwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu yote, 216 kwa kipengele cha juzuu tano, na 88 kwa kipengele cha juzuu kumi. Vipengele na njia nyingine pia zilitolewa ili kukidhi makundi mbalimbali ya umri na viwango vya kuhifadhi na kusoma Qur’ani, zikiwemo njia maalum kwa raia wakongwe wa Kiemirati na Waislamu wapya.
3499635