IQNA – Takwimu za Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) zinaonyesha mtindo maalumu: uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo la Minnesota nchini Marekani huongezeka wakati wa miaka ya uchaguzi.
Tangu 2016, takwimu za FBI zinaonyesha kuwa uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo hilo umekuwa ukiongezeka katika miaka ya uchaguzi wa katikati ya muhula na uchaguzi wa rais. FBI inasema kuwa kumezuka matukio 12 ya uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu katika jimbo hilo hadi sasa mwaka huu. Viongozi wa Kiislamu wanachukua hatua za kulinda usalama wa jamii zao, na kuhimiza wananchi kujitokeza kupiga kura.
Imamu Abdulahi Farah alishuhudia msikiti wake ukigeuka kuwa eneo la uhalifu miaka tisa iliyopita. Sasa, kabla ya uchaguzi wa Jumanne Novembe 3 unapokaribia na matamshi ya kisiasa yanayowalenga Wasomali wa Minnesota yakizidi kushika kasi, yeye na viongozi wengine wa Kiislamu wanaimarisha usalama tena.
“Tunatamani tungelikuwa katika mazingira ambayo si lazima tufanye haya yote, lakini kutokana na hali inayotengenezwa sasa, haya ni mambo ambayo lazima tufanye. Tunapaswa kuzungumza na vijana kuhusu kujilinda na mambo kama hayo,” alisema Farah.
Kufikia sasa mwaka huu, kumezuka matukio 12 ya uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu katika jimbo hilo, yakiwemo mawili katika misikiti, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na FBI. Mwezi uliopita, tawi la Minnesota la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) liliandaa mkutano kwa ajili ya maimamu na viongozi wa dini nyingine ili kuzungumzia mipango ya kiusalama.
Farah ni imamu katika Msikiti wa Dar Al-Farooq ulioko Bloomington. Mnamo 2017, watu watatu kutoka kundi lenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia walishambulia ofisi yake kwa bomu la petroli katika shambulizi dhidi ya msikiti huo. Hakuna aliyeruhiwa, akiwemo watu watano waliokusanyika kwa ajili ya sala ya mapema asubuhi hiyo.
Hofu kubwa ya Farah ni kwamba jambo hilo linaweza kutokea tena.
“Nadhani kitu kibaya zaidi ni pale watu wanapojitenga na misikiti kwa sababu ya hofu,” alisema.
Kwa miaka mingi, msikiti umeekeza katika hatua nyingi za usalama, zikiwemo madirisha yasiyopenya risasi, kamera, na walinzi wa usalama. Polisi pia wamefanya vikao vya mafunzo ili kuwafundisha jinsi ya kukabiliana na vitisho. Farah alisema kuajiri walinzi wa usalama kunawagharimu maelfu ya dola kila mwaka.
Ingawa Farah hakutaka kutoa maelezo ya kina kwa sababu hataki kuitisha jamii, alisema Msikiti wa Dar Al-Farooq umepokea vitisho kadhaa mwaka huu.
Hudhayfa Suhail, imamu katika Msikiti wa Lakeville, alisema takwimu za FBI hazionyeshi picha kamili, kwa sababu anaamini uhalifu wa chuki hauripotiwi ipasavyo na Waislamu na baadhi ya misikiti.
Kinyume chake, Msikiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Amerika huko Blaine haujapokea vitisho vyovyote hivi karibuni, kulingana na Jawad Islam, kiongozi ndani ya msikiti huo. Licha ya ukosefu wa vitisho, alisema usalama bado ni kipaumbele kikubwa, huku kukiwa na kamera kuzunguka jengo hilo, madirisha yasiyopenya risasi katika ukumbi wa sala, na uwepo wa polisi wakati wa sala ya Ijumaa ili kudhibiti msongamano wa magari.
3499646/