IQNA – Kundi la wanaume na wanawake wa Algeria waliohifadhi Qur’ani Tukufu limetunukiwa katika hafla maalum iliyofanyika nchini humo, likizawadiwa safari ya kwenda kutekeleza ibada ya Umra.
Kwa mujibu wa mtandao wa IUMSonline, ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wananchi katika mji wa Ain Oussara, ulioko kusini-kati mwa Algeria, ulikuwa wenyeji wa hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwa ajili ya kuwaenzi na kuwapongeza wanaume na wanawake waliofanikiwa kuhifadhi Qur’ani.
Hafla hiyo iliadhimisha kuhitimishwa kwa msimu wa shughuli za Qur’ani kwa mwaka 1448 Hijria (2026 Miladia) na iliandaliwa na taasisi ya Algeria ya “Harakati Pamoja na Qur’ani” (Movement with the Quran).
Programu hiyo ilihudhuriwa na wanazuoni wa Qur’ani, wahubiri, na wasomi mbalimbali, ambapo ilianza kwa kisomo kitukufu cha Qur’ani kilichotolewa na Sheikh Yassin Amran.
Sheikh Ibrahim Lamouri, mkuu wa taasisi hiyo, alihutubia mkutano huo. Huku akinukuu Aya ya 58 ya Surah Yunus, alisisitiza kuwa moja ya mafanikio makubwa zaidi ambayo mwanadamu anaweza kuyafikia ni kuhifadhi Neno la Mwenyezi Mungu, kujenga uhusiano wa dhati na Qur’ani, na kuenenda kwa maadili ya Qur’ani katika maisha ya kila siku.
Aliongeza kuwa lengo lenye thamani kuu ambalo mtu anaweza kutoa rasilimali zake kwa ajili yake ni kueneza Qur’ani miongoni mwa jamii na kuimarisha uwepo wake katika maisha yao ya kila siku.
Wakati wa hafla hiyo, wanazuoni na waelimishaji walitoa hotuba zilizosifu juhudi na msimamo thabiti wa wale wote waliofanikiwa kuhifadhi Qur’ani nzima. Walisisitiza fadhila kuu za kuwa na uhusiano wa karibu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambao hupatikana kupitia kuhifadhi, kutafakari, na kutumia kivitendo mafundisho yake.
Pia waliwahimiza mahufadhi hao kuendelea na safari yao ya Qur’ani, kujitahidi kutafuta elimu zaidi, na—kwa kujipamba kwa maadili ya Qur’ani—kuwa vielelezo vyema katika kulitumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kueneza mafundisho yake.
Kama ishara ya kuthamini juhudi zao kubwa katika njia ya Qur’ani, mahufadhi na walimu 65 walisafirishwa kwenda kutekeleza ibada ya Umra, msaada uliotolewa kupitia michango ya wadau na wahisani wema.
Taasisi ya Movement with the Quran ni shirika la kidini lisilo la faida lenye makao yake nchini Algeria. Linafanya kazi kwa lengo la kueneza uhifadhi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, likiongozwa na kauli mbiu: “Tunaishi pamoja na Qur’ani, na kwayo tunapanda juu.”
3499644