IQNA

19:35 - November 03, 2026
Habari ID: 3482994

Mwanaharakati wa Jamhuri ya Azerbaijan anayepinga marufuku ya Hijabu mashuleni ateswa gerezani

IQNA – Mwanaharakati wa kijamii nchini Jamhuri ya Azerbaijan amepigwa na kuteswa akiwa kizuizini kufuatia maandamano yake ya kupinga marufuku ya vazi la Hijab katika shule za nchi hiyo.

h

Tovuti ya Kavkazsky Uzel iliripoti kuwa Yavar Ismayilzadeh, mwanaharakati Mwislamu anayehusishwa na vuguvugu la “Umoja wa Kiislamu” la Jamhuri ya Azerbaijan, alipigwa na kutishiwa akiwa ameshikiliwa katika gereza moja nchini humo.

Kwa mujibu wa watu wa karibu naye, tukio hili lilitokea baada ya mwanaharakati huyo kuanzisha mgomo wa njaa mnamo Oktoba 14 kwa ajili ya kupinga marufuku inayowazuia wanafunzi na walimu kuvaa hijab mashuleni.

Matukio haya yanajiri kufuatia maandamano yaliyozuka baada ya vikwazo vinavyohusu hijab mashuleni kuwekwa tarehe 12 Oktoba. Wakati mamlaka zikidai kuwa zimewakamata watu 37 pekee, wanaharakati wanakadiria kuwa idadi ya waliowekwa kizuizini inazidi watu 200.

Chanzo cha vikwazo hivi kinatokana na marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Elimu ya Ujumla mnamo Julai 2026, ikifuatiwa na maazimio yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri mnamo Septemba 21 na Oktoba 6 mwaka huo.

Ingawa neno hijab halijatajwa waziwazi katika maandishi ya maazimio hayo, yanapiga marufuku aina yoyote ya vazi linalochukuliwa kuwa “lisilooana na usawa wa sare za shule au kanuni ya sekula katika elimu ya umma.”

Kiutendaji, kanuni hizi zimesababisha wanafunzi na walimu wanaovaa hijab kuzuiwa kuingia katika maeneo ya shule. Kusambaa kwa video zinazowaonyesha wasichana waliovaa hijabu wakinyimwa ruhusa ya kuingia mashuleni mwao kumezua wimbi la maandamano mjini Baku na katika miji ya kusini mwa nchi hiyo.

Serikali ya Azerbaijan inatetea uamuzi huu kwa kutaja katiba ya nchi hiyo, ambayo inafafanua mfumo wa elimu kuwa wa sekula. Hata hivyo, wakosoaji, wakiwemo shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, wanaona hatua hiyo kuwa ya ubaguzi na ukiukaji wa wazi wa haki ya kupata elimu na uhuru wa kidini kwa wasichana wa Kiislamu.

3499645

captcha