IQNA

17:34 - November 04, 2026
Habari ID: 3483000

Kiongozi asisitiza kuhusu Iran “yenye nguvu zaidi daima”, asema ni njia pekee ya kuwazuia maadui

IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Mojtaba Khamenei, amesema kuendelea na mkakati wa kuifanya Iran “iwe na nguvu zaidi daima” kupitia maendeleo ya kila nyanja ndiyo njia pekee ya kufikia “uwezo kamili wa kumzuia adui” (absolute deterrence).

yatollah Seyed Mojtaba Khamenei

Katika ujumbe wa Jumatano wa kuadhimisha Novemba 4, Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Uistikbari Kimataifa nchini Iran, Kiongozi amsisitiza kwamba umoja wa kitaifa, muungano na mshikamano wa kijamii lazima vitawale mwenendo wa taifa la Iran na viongozi wake.

Kiongozi amesema uungwaji mkono wa wananchi kwa viongozi ni jambo la lazima, huku akisisitiza kwamba mamlaka lazima ziendelee kuongeza umakini wao katika “huduma ya bidii, ya kujitolea na ya dhati,” kuwa karibu na wananchi, kuhakikisha riziki na ustawi wao, kuendeleza ukuaji wao wa kimali na wa kiroho, na kulinda utu na uhuru wao.

Ayatullah Mojtaba Khamenei amesema muqawama wa taifa la Iran umeufikisha mzozo na Marekani katika hatua ambapo si Novemba 4 pekee, bali “siku na saa zote” zimekuwa siku za kusimama imara na kupambana na “Shetani Mkuu.”

Akizungumzia matukio katika Ghuba ya Uajemi, hasa Lango-Bahari la Hormuz, Ayatullah Khamenei amesema hali hiyo imeonyesha “uongo wa ngano ya kutoshindika kwa Marekani.”

Amesema pia matukio hayo yamefichua “udhaifu na unyonge wa serikali zinazotegemea nguvu nyingine isiyo ya watu wao wenyewe, pamoja na ukosefu wa uaminifu na uwezo wa mataifa makubwa katika kutetea serikali tegemezi kwake.”

Amesema, “Udhibiti wa Iran juu ya Lango-Bahari wa Hormuz na kuharibiwa kwa kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za kanda hii, ingawa ni jibu kwa uchokozi na uhalifu wa Marekani katika vita vya tatu vilivyolazimishwa, pia ni jihadi ya awali dhidi ya uistikbari kimataifa katika kiwango cha kanda.”

Ameonya kwamba “endapo uchokozi huu utarudiwa, vipimo vyake vitakuwa pana zaidi.”

Kiongozi ameyaelezea matukio haya, pamoja na umoja wa Mhimili wa Muqawama na hatua za busara na zenye nguvu za harakati za mapambano kuanzia Palestina na Lebanon hadi Iraq na Yemen, kuwa “alfajiri angavu yenye kutia matumaini” kwa kuinuliwa kwa safu ya haki na kuasisiwa kwa mfumo mpya wa dunia.

Amesema, “Wakati wowote safu ya haki inapokuwa na imani kwa Mungu, subira na kujitolea mhanga, safu ya batili, vyovyote vile nguvu na uwezo wake, haitaweza kuistahimili, na kurudi nyuma na kushindwa ndiko kutakuwa hatima yake isiyoepukika.”

Ayatullah Khamenei aliwaambia wale wanaoendelea kutumaini mabadiliko ya tabia ya Marekani kwamba:  “Ikiwa bado wapo wenye matumaini hata kidogo ya mabadiliko ya tabia au ya mabadiliko ya kisiasa na ya kivyama ndani ya mfumo wa utawala wa kibabe, au wanaodhani kwamba kwa kulegeza msimamo mbele ya Marekani wanaweza kuizuia kuacha uadui wake dhidi ya taifa la Iran, basi wamekosea vibaya sana.”

Akielezea matarajio kama hayo kuwa ni kupuuza ushindi mkubwa uliopatikana na wananchi wa Iran kwa kumtegemea Mungu, subira na mapambano, amesema lengo kuu la “Shetani Mkuu” ni taifa la Iran kujisalimisha bila masharti.

Ameongeza kuwa, “Hata mwelekeo mdogo kabisa wa kujisalimisha mbele ya adui mkandamizaji utapoteza mtaji mkubwa uliopatikana kwa damu ya mashahidi na kujitolea kwa makundi yote ya taifa, na utamtia ujasiri adui mwenye kiburi kutoa madai mengine ya kupindukia na kufanya vitendo zaidi vya uchokozi na vita.”

Katika kupitia historia ya uadui wa Marekani dhidi ya Iran, Ayatullah Khamenei alifuatilia chanzo chake hadi zaidi ya miongo saba iliyopita, akitaja mapinduzi ya Agosti 1953 kuwa mwanzo wa dhuluma ya Marekani dhidi ya taifa la Iran.

Amesema mapinduzi hayo yalipangwa ili kuhakikisha uporaji wa rasilimali na utajiri wa taifa la Iran, hasa mafuta yake, unaendelea.

Alisema, “Miongo iliyofuata, hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nayo ilikuwa kipindi ambacho watawala wa Marekani walifanya juhudi kubwa za kupora mali za taifa la Iran.”

Ayatollah Khamenei amesema Washington ilianzisha shirika la kijasusi la SAVAK na kuweka hali nzito ya kiusalama katika jamii ya Iran, na hivyo kuipa serikali ya wakati huo uhuru mkubwa zaidi wa kukandamiza harakati yoyote ya maandamano.

Ameongeza kwamba, usiku wa kuamkia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ilitumia mipango mbalimbali kulinda serikali yake tegemezi.

Kiongozi amesema orodha ndefu ya vitendo dhidi ya Iran inaweza kuwasilishwa kutoka kipindi kilichofuata ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Miongoni mwa vitendo hivyo, alitaja uungaji mkono wa Marekani kwa makundi ya kutaka kujitenga, makundi ya waliopanga kuupindua mfumo wa Kiislamu, na kundi la kigaidi la MKO, ambalo amesema limeua kikatili idadi kubwa ya watu wa kawaida, mbali na watu mashuhuri wa kisayansi, kisiasa na kijamii.

Pia alitaja uungaji mkono kamili wa Marekani kwa utawala wa Kibaath wa Saddam Hussein wakati wa vita vya kwanza vilivyolazimishwa vya mwaka 1980-1988, kuuawa kwa abiria waliokuwa ndani ya ndege ya kiraia ya Iran, vikwazo vya kiuchumi vya kina na vya muda mrefu, kupanga na kuunga mkono ghasia na fitna za mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kuzisaidia kwa silaha, pamoja na mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, ambaye alimweleza kuwa shujaa wa kitaifa wa Iran na wa Umma wa Kiislamu.

Kushikiliwa kwa mali za wananchi wa Iran katika nchi mbalimbali pia kulikuwa miongoni mwa vitendo alivyovitaja.

Ayatullah Khamenei aliilenga zaidi Marekani kwa uchokozi wa moja kwa moja wa kijeshi wakati wa vita vya pili na vya tatu vilivyolazimishwa, ambavyo vilisababisha kuuawa kishahidi kwa watu wengi mashuhuri, wanasayansi na makamanda, pamoja na idadi kubwa ya Wairani wa kawaida, kuanzia watoto wachanga na wadogo hadi wazee.

Alimtaja Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, kuwa wa kwanza kabisa miongoni mwa waliouawa.

Amesema, “Katika kila hatua, watawala wenye kiburi wa Marekani na wafuasi wao wamekuwa wakijaribu daima kulazimisha utawala wao na kuilazimisha Iran kujisalimisha.”

Ameongeza kuwa Washington sasa imetupilia mbali hata taratibu za kimaonyesho katika uga wa kimataifa, na inafuatilia waziwazi kuigawa Iran vipande vipande, kujisalimisha kwa watu wake, kuanguka kwa mfumo wake wa kisiasa na kuharibiwa kwa ustaarabu wake wa kale na halisi.

Hata hivyo, Ayatullah Khamenei amesema, Marekani imekumbana na “ukuta imara wa uhalisia wa uwanjani na mwamba thabiti wa azma ya taifa la Iran lenye heshima” katika kila hatua.

Amesema matokeo ya hesabu potofu za Marekani na ndoto zake za kiburi yameliletea gharama kubwa taifa la Marekani na serikali zinazoitegemea Washington.

Ayatullah Khamenei amesema Muqawama wa wananchi wa Iran umefikia hatua ambapo mzozo na Marekani umekuwa mapambano ya kila siku yasiyokoma.

Aidha amesema matukio katika Ghuba ya Uajemi na hatua za Mhimili wa Muqawama kuwa ishara za kudidimia kwa utawala wa Marekani na kuibuka kwa mfumo mpya wa kimataifa.

Amesema, “Leo, kutokana na aibu ya kujitakia ya madola yenye kiburi, nguvu na utawala wa Marekani unaodidimia, upande wake wa nguvu ngumu ya kijeshi na wa nguvu laini ya kimataifa, umeanguka anguko lisilorudishika, na mchakato wa kuporomoka kwake umeharakishwa.”

Kiongozi amesema umoja wa safu ya haki, pamoja na kujitolea na subira ya harakati za mapambano katika kanda nzima, unatoa mwelekeo wa matumaini kwa ushindi wa mwisho wa safu hiyo.

Akirejea masharti ya kuiimarisha Iran, Ayatullah Khamenei alisisitiza kwamba umoja wa kitaifa na mshikamano wa kijamii lazima uonekane katika mwenendo wote wa mtu binafsi na wa pamoja.

Amesema kwamba ingawa uungwaji mkono wa wananchi kwa viongozi ni wa lazima, mamlaka zina jukumu la kuongeza juhudi zao za kuwahudumia wananchi, kujenga ukaribu zaidi nao na kuhakikisha ustawi wao wa kimali na wa kiroho.

Amesisitiza hasa haja ya kuhakikisha mahitaji ya kila siku ya wananchi yanatimizwa, kuendeleza maendeleo yao na kulinda utu na uhuru wao.

Ayatullah Khamenei aliwataja vijana, wanafunzi wa vyuo vikuu na watoto wa shule kuwa nguvu kuu ya kujenga mustakabali mwangavu na wenye utukufu kwa Iran.

Alisema lazima wafanye kazi kwa kuendelea kuushinda na kuubomoa ngome ya giza ya “kukata tamaa, kutokuwa na matumaini na kutowezekana”, na kuchukua udhibiti wa makazi angavu ya “matumaini na tunaweza.”

Amesema, “Sharti la dhima hii ni maandalizi ya kipekee na kujizatiti kwa silaha mbalimbali za elimu, uchamungu, ujuzi, maadili, azma na juhudi za ajabu, pamoja na kujitolea kwa pamoja kufikia malengo makubwa.”

Kiongozi amesema taifa la Iran limejifunza mafunzo makubwa kutoka mafundisho ya Uislamu, kanuni za Mapinduzi ya Kiislamu na fikra za viongozi wake wenye hekima, Imam Khomeini na Shahidi Ayatllah Khamenei.

Amesema kwamba, kupitia kutimia kwa ahadi za Mwenyezi Mungu, imani ya wananchi wa Iran katika uhalali wa njia hii imezidi kuimarika siku hadi siku.

Ayatullah Khamenei amesema subira ya taifa la Iran, kumtegemea Mungu na kujitolea kwake kuwa msingi wa mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na Marekani na mfumo wa utawala wa kibabe.

Kiongozi wa Mapinduzi amebainisha matumaini kwamba, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na dua za Imam wa Zama, taifa la Iran litapata hivi karibuni ushindi, ustawi na maendeleo ya kila nyanja, huku kudidimia kwa utawala wa “Shetani Mkuu” kukiharakishwa.

Akinukuu Qur’ani (Surat Al-Ma’arij, aya 6–7), alisema: “Hakika wao wanaiona iko mbali, nasi tunaiona iko karibu.”

3499671

captcha