IQNA

Waislamu Tanzania wataka uchunguzi kuhusu maafa ya Mina

20:37 - October 03, 2015
Habari ID: 3377983
Waislamu nchini Tanzania wametaka iundwe kamati ya kimataifa kuchunguza maafa ya hivi karibuni huko Mina karibu na mji mtukufu wa Makka ambapo zaidi ya Mahujaji 5,000 walipoteza maisha.

Wakizungumza Alhamisi mjini Dar es Salaam, viongozi wa Kiislamu walisema usimamizi mbovu ndio uliopelekea vifo vya Mahujaji huko Mina wakati wa siku kuu ya Idul Adha.
"Usimamizi mbovu ndio chanzo kikuu cha mkannyagano uliojiri Mina Septemba 24," alisema Sheikh Abdulmalik Almas ambaye alishiriki katika Ibada ya Hija mwaka huu na kunusurika maafa ya Mina. Ameukosoa utawala wa Saudia kwa kuwaluamu mahujaji 'Waafrika' kuwa ndio waliosababisha  maafa ya Mina kwa madai kuwa hawakuzingatia kanuni zilizowekwa.
Kauli ya Sheikh Almas pia iliungwa mkono na Alhajj Abdul Kaway ambaye pia alinusurika maafa ya Mina na kusema alishuhudia maafisa wa usalama Saudia wakifunga njia iliyokuwa ikitumiwa na mahujaji waliokuwa wakirejea baada ya kumaliza amali ya kumpiga mawe shetani eneo la  Ramy al-Jamarat na kuwalazimu watumie njia walimokuwa Mahujaji waliokuwa wakielekea eneo hilo jambo ambalo lilipelekea kugongana makundi hayo mawili na kusababisha maafa makubwa.
Aidha ametoa wito kwa serikali ya Tanzania ikague usajili wa mawakala huku akisema baadhi wannasimamizi visivyo masuala ya Hija.
Naye Sheikh Ghawth Nyambwe mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al Mustapah SAW amesema kuna haja ya kuundwa kamati ya kimataifa kuchunguza usimamizi mbovu wa Saudia katika kadhia ya Mina.
Maafisa wa serikali ya Tanzania wamethibitisha kuwa mahujaji watano wa nchi hiyo waliaga dunia Mina huku wengine 50 wakitoweka.
Kwa ujumla Watanzania takribani 3,000 wakiwemo 1,300 kutoka Zanzibar walishiriki katika ibada ya Hija mwaka huu.../mh

3377890

captcha