IQNA

Mashia 5 wauawa Saudia katika hujuma ya ISIS

6:02 - October 17, 2015
Habari ID: 3386096
Waislamu watano wa madhehebu ya Shia wameuawa nchini Saudi Arabia kufuatia hujuma ya kundi la kigaidi la Daesh au ISIS katika majlisi ya maombolezo ya siku 10 za Muharram.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Saudia, watu tisa pia walijeruhiwa wakati gaidi aliyekuwa na bunduki aliposhambulia ukumbi wa kidini ujulikanao kama Husseiniya katika wilaya ya Al Kawthar mjini Saihat karibu na eneo la Qatif mashariki mwa Saudi Arabia. Televisheni ya al-Ekhbariya imesema kuwa, Ijumaa usiku kijana mwenye umri wa takribani miaka 20 hivi alishambulia Husseiniya kwa risasi na kuua watu watano. Aidha ripoti zinasema gaidi huyo aliuawa na vikosi vya Saudia katika eneo  hilo. Kundi la kigaidi la ISIS limekiri kuhusika na hujuma hiyo. Wakati wa hujuma hiyo, Waislamu wa madhehebu ya Shia walikuwa wanaendelea na vikao au majlisi za mwezi wa Muharram ambao kilele chake ni siku ya 10 ijulikanayo kama Ashura wakati Waislamu hukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mtume Muhammad , SAW, Imam Hussein AS huko Karbala. Baada ya hujuma hiyo mjini Saihat, idadi kubwa ya watu waliandamana kulaani vitendo vya kigaidi dhidi ya Waislamu wa Kishia.  Katika miezi ya hivi karibuni magaidi wa ISIS wamekuwa wakitekeleza mashambulio dhidi ya misikiti ya Mashia mashariki mwa Saudi Arabia. Magaidi wa ISIS wameteka maeneo makubwa ya ardhi Syria na Iraq huku wakieneza ugaidi wao katika nchi zingine kama vile Libya na Misri. Serikali ya Syria inailaumu Saudi Arabia kuwa ndie muungaji mkono mkuu wa magaidi wa ISIS.../mh

3386073

captcha