IQNA

Taarifa ya mwisho ya mkutano wa Tehran kuhusu Palestina

Waislamu na wapenda haki duniani waungane kusaidia ukombozi wa Palestina

23:22 - February 22, 2017
Habari ID: 3470864
IQNA-Taarifa ya mwisho ya Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina uliomalizika leo hapa mjini Tehran limesisitizia udharura wa kulindwa kadhia ya Palestina ambayo ni kipaumbele cha kwanza cha nchi ulimwengu wa Kiislamu na za Kiarabu na ndilo zingatio kuu la fikra za walio wengi duniani.

Katika taarifa yao ya mwisho, washiriki wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina wamemshukuru Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa miongozo yake ya hekima wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kusema kwamba, umoja wa taifa la Palestina na kukubali kuwa muqawama ndilo chaguo pekee la kukomboa haki za taifa hilo hasa kwa kuzingatia kuwa mafanikio ya muqawama yameonekana katika ukombozi wa kusini mwa Lebanon na Ukanda wa Ghaza kama ambavyo pia umeonesha nguvu zake za kukabiliana na tamaa za adui.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Safu za umma wa Kiislamu na mataifa ya wapenda ukombozi duniani zinapaswa kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kulisaidia taifa madhlumu la Palestina".

Aidha tamko hilo limesema, Intifadha na mapambano au muqawama wa taifa madhlumu la Palestina hususan mapambano ya hivi sasa ndiyo njia pekee ya maana katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Washiriki wa mkutano huo wa kimataifa aidha wametilia mkazo wajibu wa kuendelezwa juhudi za kumaliza jinai ya utawala wa Kizayuni wa kuikalia kwa mabavu Palestina, kulindwa ardhi yote ya kihistoria ya Palestina inayoanzia baharini hadi mtoni na kuundwa dola la Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.

Katika taarifa hiyo ya mwisho, washiriki wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina wameitaka jamii ya kimataifa kuushinikiza vilivyo utawala wa Kizayuni ili uache vitendo vyake visivyo vya kibinadamu ikiwemo kuuzingira kidhulma Ukanda wa Ghaza.

 Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina uliomalizika leo Jumatano hapa Tehran, umeshirikisha ujumbe zaidi ya 80 wenye washiriki zaidi ya 700 kutoka kona zote za dunia.

Mkutano huo ambao nara yake kuu ilikuwa ni , "Wote kwa Pamoja katika Kuunga Mkono Palestina" uliwaleta pamoja maspika wa mabunge, wabunge, waku wa tume za sera za kigeni katika mabunge, wasomi na wanasiasa wa ngazi za juu, wanaharakati wa kupigania ukombozi Palestina na mashirika yasiyo ya kiserikali yenye kutetea Palestina kote duniani.

3577440


captcha