IQNA

Shirika la Reli Japan lajenga vyumba vya Waislamu kuswali katika kituo muhimu

0:29 - April 30, 2018
Habari ID: 3471489
TEHRAN (IQNA)- Shirika moja la reli nchini Japan limejenga vyumba vya Waislamu kuswali katika moja ya vituo vyake muhimu.

Shirika la Reli la Tobu mnamo Aprili Mosi ililifungua vyumba vya kuswali katika Kituo cha Tobu Nikko kwa lengo la kuwavutia zaidi Waislamu wanaosafiri kutoka nchi za kusini mashariki mwa Asia kama vile Malaysia na Indonesia. Nikko ni mji mdogo katika jimbo la Tochigi kaskazini mwa mji mkuu wa Japan, Tokyo.

Kwa mujibu wa taarifa, vyumba hivyo viwili, kimoja cha wanaume na kingine cha wanawake, viko katika  ghorofa ya pili ya Kituo cha Tobu Nikko. Kituo hicho kina suhula za kuwawezesha Waislamu kushika wudhuu. Shirika la Reli la Tobu pia lina hoteli maalumu ambazo huwahudumia watalii Waislamu kwa kutoa huduma za chakula halali.

Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Utalii Japan, mwaka 2017 kulikuwa na watalii milioni 28.69 wa kigeni waliotembelea nchi hiyo. Watalii Waislamu pia wanazidi kuongezeka Japan kila mwaka na kwa msingi huo mashirika ya kutoa huduma yanajitahidi kuwaandalia Waislamu suhula za kuwawezesha kusafiri kwa kizingatia mafundisho ya Uislamu.

3465671

captcha