IQNA

Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Kadhia ya kupewa sumu wanafunzi ni uhalifu mkubwa

18:22 - March 06, 2023
Habari ID: 3476666
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kadhia ya kupewa sumu wanafunzi hapa nchini ni uhalifu mkubwa na haiwezi kuachiwa.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo leo pembeni ya hafla ya upandaji mti alipozungumzia kadhia ya kupewa sumu wanafunzi, ambapo sambamba na kusisitiza kuwa viongozi husika na vyombo vya intelijensia na polisi inapasa vilifuatilie suala hilo kwa uzito mkubwa amesema: kadhia hii ni uhalifu mkubwa na haiwezi kuachiwa, na kama kutakuwa na watu wamehusika inapasa waliohusika na wasababishaji wake wapewe adhabu kali kabisa.

Ayatullah Khamenei amesema, suala hilo ni jinai dhidi ya watu wasiofanya makosa zaidi katika jamii, yaani watoto, na pia linasababisha kuvurugika usalama wa kisaikolojia wa jamii na kuzitia wasiwasi familia, na akasisitiza kuwa: watu wote wajue kwamba, ikiwa kuna watu watabainika na kutiwa hatiani, hakuna msamaha wowote utakaotolewa kwao kwa sababu itapasa wapewe adhabu kali kabisa ili liwe funzo kwa wengine.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ametaja pia sababu ya kupanda miche mitatu kwa kauli mbiu ya Siku ya Upandaji Miti ya "Miche Mitatu kwa kila Muirani" na kusema: Iwapo kila Muirani atapanda miche mitatu kwa kuzingatia kauli mbiu iliyochaguliwa, basi mpango wa serikali wa kupanda miche bilioni moja kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka1402 utafanikiwa.

Ayatullah Khamenei ameashiria umuhimu wa kupanda miche katika kuhifadhi mazingira na kusisitiza kwamba kwa msaada wa wananchi lengo la kupanda miche bilioni moja linaweza kufikiwa. Aidha ameongeza kuwa: ushauri wa mabingwa na wataalamu ni kwamba pamoja na kupanda miti ya matunda, ipandwe pia miti ya misitu na miti ambayo mbao zake zina umuhimu, kwa sababu biashara ya mbao ina athari kubwa katika uchumi wa nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amekumbusha pia kwamba, matokeo ya kuwa na uchumi unaotegemea pato la kitu kimoja tu ndio hali inayoshuhudiwa hivi sasa ambapo nchi ina matatizo ya  thamani ya sarafu ya taifa, kupanda bei za bidhaa na ughali wa maisha.

4126360

captcha