IQNA

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria apelekwa kusikojulikana

17:52 - December 11, 2016
Habari ID: 3470735
IQNA-Duru kutoka Nigeria zinadokeza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amehamishiwa sehemu isiyojulikana nchini humo.

Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeripoti leo Alfajiri kwamba kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akiwa na mke wake wamechukuliwa sehemu waliyokuwa wakizuiliwa na askari usalama wa nchi hiyo na kupelekwa kusikojulikana. Habari hiyo imethibitishwa pia na Ibrahim Musa, msemaji wa harakati hiyo ya Kiislamu ambaye ameitahadharisha serikali ya Nigeria akisisitiza kuwa itabeba dhima ya jambo lolote litakalomfika kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu.

Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake alitiwa mbaroni na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka uliopita katika kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria kaskazini mwa jimbo la Kaduna ambapo mamia ya Waislamu waliouawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika tukio hilo. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

captcha