IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran inaweza kuvuka njia ngumu za maendeleo ya ustawi kupitia mchango athirifu wa elimu na malezi

19:05 - May 02, 2023
Habari ID: 3476949
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na idadi kubwa ya walimu nchini Iran na akasema: Ni jambo lisilowezekana kuvuka njia ngumu za maendeleo ya pande zote ya nchi bila ya msaada na mchango wa sekta ya elimu na malezi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei leo Jumanne amezungumza mbele ya hadhara ya walimu katika hafla ya kumkumbuka siku ya alipouawa Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhari, ambayo ni Siku ya Mwalimu nchini Iran. Kiongozi Muadhamu amemtaja Shahidi Mutahhari kuwa ni kielelezo cha mwalimu mkweli na aliyekamilika katika fani yake; na kuwanasihi walimu kutumia vyema athari na kazi za msomi huyo. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa: Kuhuishwa hisia za utambulisho wa Kiirani na Kiislamu na hadhi ya utaifa miongoni mwa vijana na mabarobaro weledi wa nchi hii, ni jukumu muhimu la kimsingi na kwamba katika mchakato huo, suala la lugha ya Kifarsi, bendera ya nchi na hisia za heshima na kujifakharfisha kwa kuwa Muirani ni jambo lenye umuhimu mkubwa; ambapo bila ya shaka masuala haya hayawezi kupatikana kwa ushauri na maneno matupu, bali wanafunzi wanapaswa kufundishwa uhakika wa mambo na kumbukumbu halisi za kiutamaduni, kisayansi na kihistoria.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kujumuishwa fikra za Kiislamu na kuarifishwa fahari za Kiislamu na Kiirani na wasomi wa kielimu na wavumbuzi wa sayansi katika historia ya Iran ni miongoni mwa kazi zinazohitajika kwa ajili ya kusasisha vitabu vya kufundishia kulingana na mabadiliko yaliyopo na kubainisha kuwa: Lengo la baadhi ya watu kuhusu kubadilika zama ni kutaka kubadilisha sheria katika hali ambayo  kanuni kama uadilifu, isnafu na mapenzi kamwe havibadiliki bali mifumo kama vile njia za kuandika na kujieleza ndio hubadilika.  

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria mabadiliko ya kimsingi ya elimu na kutoa mapendekezo matano kwa viongozi husika na kusema, Mosi, ni kuhusu hati inayohusiana na mabadiliko endelevu na yaliyokamilika ambayo yanapasa kusasishwa, Pili, ni kuhusu waraka wa mageuzi yanayopaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na kusaidia katika utekekelezaji wake, Tatu, kusiwe na mbadala au ushindani wa waraka wa mabadiliko ambao ni waraka thabiti na mzuri, Nne,  iandaliwe ramani ya njia sahihi ya kutekeleza hati ya mabadiliko kuanzia makao makuu hadi mashuleni na iungwe mkono na Serikali na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), na Tano, viashiria vinavyoweza kupimika vinapaswa kuamuliwa kulingana na upigaji hatua mchakato wa utekelezaji wa hati na hivyo kuweza kufuatiliwa ipasavyo. 

4137911

captcha