IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Chama cha Wanasheria Marekani Chahimiza Bunge, Umoja wa Mataifa kukabiliana na chuki dhidi Uislamu

18:42 - August 10, 2023
Habari ID: 3477413
WASHINGTON, DC (IQNA) - Baraza la Chama cha Wanasheria wa Marekani (ABA), chombo kikubwa zaidi cha wanasheria nchini Marekani, kimepitisha azimio la kulaani chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Pia baraza hilo limetoa wito kwa Bunge la Marekani, Congress,  na Umoja wa Mataifa kupitisha maazimio sawa ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu
Baraza la Chama cha Wanasheria wa Marekani (ABA), lilipitisha azimio hilo siku ya Jumanne wakati wa kikao cha siku mbili kikiangalia sera na maazimio mengi mapya.
"Imeamuliwa, Kwamba Chama cha Wanasheria wa Marekani kinazitaka serikali za shirikisho, majimbo, mitaa, maeneo na makabila nchini Marekani kulaani chuki dhidi ya Uislamu na kuandaa na kutekeleza mikakati kamili ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu," azimio hilo lilisema.
Mikakati iliyopendekezwa iliyotajwa katika azimio hilo ni pamoja na kuunda kampeni za kuwaelimisha Wamarekani kuhusu Uislamu na Waislamu na pia mbinu mpya za kuripoti matukio ya chuki dhidi ya Uislamu na uhalifu wa chuki.
Azimio hilo pia linahimiza Bunge la Marekani kupitisha mswada uliowasilishwa na Mbunge Ilhan Omar wa kuanzisha ofisi katika Wizara ya Mambo ya Nje ambayo inafuatilia chuki dhidi ya Uislamu - sawa na ile iliyopo ya kufuatilia chuki dhidi ya Wayahudi.
Sheria hiyo bado haijapata kura kwenye  Congress.
Mashirika ya Kiislamu kwa miaka kadhaa yameitaka Marekani kufuatilia suala la chuki dhidi ya Uislamu nchini humo, na pia yameushawishi Umoja wa Mataifa kufanya hivyo.
Mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulipiga kura kuadhimisha "Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki Dhidi Uislamu". Lakini pamoja na hayo mwezi Machi, muungano wa zaidi ya makundi 12 ya Waislamu ulilitaka Umoja wa Mataifa kufanya zaidi kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu katika ngazi ya kimataifa.

/3484717

Habari zinazohusiana
captcha