IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu Uingereza

Chuki dhidi ya Uislamu imeshadidi Uingereza wakati wa vita vya Israel dhidi ya Gaza

21:39 - February 23, 2024
Habari ID: 3478403
IQNA - Idadi kubwa ya matukio ya chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu yameripotiwa nchini Uingereza tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza, kulingana na kundi linalofuatilia visa kama hivyo.

Taasisi ya Tell MAMA, ambayo hufuatilia taarifa za chuki dhidi ya Uislamu, imesema ilirekodi matukio ya chuki dhidi ya Uislamu yapatayo 2,010 kati ya Oktoba 7, 2023 na Februari 7, 2024. Hiyo ilikuwa zaidi ya mara tatu ya matukio 600 yaliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 335.

Kundi hilo limesema "lina wasiwasi mkubwa" kuhusu namna mzozo wa Gaza unavyochochea uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Uingereza.

Aidha Tell MAMA imewataka viongozi wa kisiasa kulaani chuki dhidi ya Waislamu na kukuza uvumilivu na heshima.

Kati ya matukio 2,010, 901 yalikuwa nje ya mtandao na 1,109 yalikuwa mtandaoni. London ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya matukio ya nje ya mtandao, ambayo yalianzia matusi na vitisho hadi kushambuliwa kimwili na uharibifu. Wanawake walikuwa waathirika wakuu, wakichangia asilimia 65 ya kesi, kundi hilo lilisema. Hii inatokana na kuwa ni rahisi wanawake Waislamu kutambuliwa kutokana na mavazi yao ya Kiislamu.

Utawala haramu wa Israel ulianza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7 baada wapiganai ukombozi wa Palestina kutekeleza Operesheni ya Mafuriko ya Kimbunga cha Al-Aqsa ili kulipiza kisasi jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Zaidi ya Wapalestina 29,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi Ukanda wa Gaza uliozingirwa huku wengi wa watu 2.4 wakiwa ni wakimbizi wa ndani.

/3487305

captcha