IQNA

Imam wa msikiti mmoja New York auawa kwa kupigwa risasi

20:28 - August 14, 2016
Habari ID: 3470522
Imam wa msikiti mmoja katika jimbo la New York nchini Marekani ameuawa kwa kufyatuliwa risasi katika hujuma ya kigaidi.

Duru za habari zinaarifu kuwa, Imam Alala Uddin Akongi wa Msikiti wa Jamia wa Al-Furqan na msaidizi wake aliyetambulika kama Thara Uddin waliuawa kwa kufyatuliwa risasi jana Jumamosi walipokuwa wakitoka kuswali swala ya Adhuhuri katika barabara ya Ozone, mji wa Borough of Queens jimboni New York.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani limelaani mauaji hayo na kusema kuwa wawili hao mbali na kuwa viongozi wa kidini, walikuwa viongozi wa kijamii katika mji huo.

Haya yanajiri wiki moja baada ya wanajeshi waliostaafu katika jimbo la Texas nchini Marekani kutishia kuwakata vichwa kwa mapanga Waislamu watakaoenda kutekeleza ibada ya swala katika Msikiti wa Al-Sahaabah mjini Wataunga jimboni hapo. Alia Salem, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani, CAIR, katika eneo la Dallas sambamba na kulaani kitendo hicho, alisema baraza hilo limekuwa likipokea malalamiko kutoka kwa wasimamizi wa msikiti huo ambao wamekuwa wakitishiwa maisha kwa njia ya simu na watu wasiojulikana.

Ikumbukwe kuwa, katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka mno nchini Marekani na barani Ulaya.

Hivi karibuni Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) alisema kuwa, kuna wasiwasi wa kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Pamoja na kuwepo propaganda chafu dhidi ya Uislamu lakini idadi ya watu wanaosilimu na kuingia katika dini hii tukufu imekuwa ikiongezeka kwa kasi mno katika ulimwengu wa Magharibi.

3460688

captcha