IQNA

13:45 - January 28, 2019
News ID: 3471823
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Kenya wamelaani vikali uamuzi wa Mahakama ya Kilele kuidhinisha marufuku ya vazi la Hijabu katika shule nchini humo huku baadhi ya viongozi wakiwataka wasichana Waislamu wapuuze uamuzi huo.

Alhamisi iliyopita, Mahakama ya Kilele Kenya ilitoa hukumu iliyosema kila shule nchini Kenya ina haki ya kuanisha  kanuni za sare. Uamuzi huo ulibatilisha uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama ya Rufaa iliyokuwa imetoa hukumu kuwa wasichana Waislamu wana haki ya kuvaa Hijabu shuleni. Mnamo Septemba 7 mwaka 2016, majaji Philip Waki, Roselyne Nambuye na Partick Kiage wa Mahakama ya Rufaa walimwagiza Waziri wa Elimu kuhakikisha sheria za shule haziwakandamizi wanafunzi kwa misingi ya dini. Uamuzi huo ulifuatia rufaa iliyowasilishwa baada ya Mahakama Kuu kuamuru kwamba hatua ya Tume ya Huduma za Walimu, TSC na serikali ya Kaunti ya Isiolo kuwaruhusu wanafunzi wa Shule ya Mseto ya St Pauls Kiwanjani, inayosimamiwa na Kanisa la Methodist, kuvalia Hijabu shuleni licha ya pingamizi ya shule hiyo ilikuwa kinyume na sheria. Kufuatia uamuzi huo Waislamu walienda Mahakama ya Rufaa na kupata ushindi. Kwa uamuzi wa Januari 24 2019, Mahakama ya Kilele Kenya imeunga mkono uamuzi wa kibaguzi wa Mahakama Kuu na hivyo kubatilisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Wasichana Waislamu watakiwa wapuuze marufuku

Kiongozi wa waliowengi katika Bunge la Kenya Aden Duale, amewataka Waislamu kupuuza uamuzi wa Mahakama ya Kilele kuhusu Hijabu. Duale amesema wasichana Waislamu wana haki kamili ya kuvaa Hijabu kwa mujibu wa katiba. Duale ambaye ni mbunge wa Mji wa Garissa amesema Majaji wa Mahakama ya Kilele hawana haki ya kupiga marufuku Hijabu kwani katiba ya nchi imebainisha wazi kuwa kila Mkenya ana uhuru na haki ya kuabudu. Wakati huo huo mratibu wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM) katika Kaunti ya Mombasa  Sheikh Shariff Muhdhar Khitamy ametoa wito wa kufanyika mazungumzo kutatua kadhia hiyo ya Hijabu. Amesisitiza kuwa Hijabu ni vazi la Kiislamu  na kulipiga marufuku ni ukiukwaji wa haki ya kikatiba ya uhuru wa kuabudu.

Amnesty International, Human Rights Watch zalaani marufuku ya Hijabu

Wakati huo huo mwakilishi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Kenya Demas Kiprono amebainisha wasiwasi wake kuwa wasichana Waislamu watapoteza haki ya masomo kutokana na marufuku ya Hijabu. Amesema Hijabu vazi  muhimu katika jamii za Waislamu na hivyo marufuku kama hiyo itapelekea baadhi ya wazazi waamue kutowapeleka wasichana wao shuleni.  Naye Agnes Odhiambo, mtafiti mwandamizi wa haki za wanawake katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema Mahakama ya Kilele Kenya imepoteza fursa ya kutoa hukumu ya kulinda haki za wanawake kuchagua vazi walitakalo. Amesema serikali inapaswa kuchukua hatua kuhakikisha kuwa wasichana Waislamu hawabaguliwi. Bi. Odhiambo amesema uamuzi  huo wa mahakama unakinzana na amani, utegamamano na kustahamiliana katika shule na jamii.

Wakenya katika mitandao ya kijamii walalamika undumakuwili

Wakenya katika mitandao ya kijamii wameshangaa ni vipi Masingasinga, Marastafari na Wakristo wa pote la Akorino wanaruhusiwa kuvaa vilemba au vitambaa lakini Waislamu wananyimwa haki hiyo. Wakili maarufu Mwislamu Ahmedassir Abdullahi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, uamuzi huo unaashiria chuki dhidi ya Uislamu walionayo majajli walipotisha hukumu ya marufuku ya Hijabu. Amesema uamuzi huo unaashiria udhaifu wa Mahakama ya Kilele nchini Kenya. Aidha Abdullahi ameshangaa ni vipi Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga alikataa kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mchana wa siku ya Jumamosi kwa sababu yeye binafsi anafuata pote la sabato linalokataza kufanya kazi Jumamosi lakini wakati huo huo mahakama anayoisimamia inawanyima wasichana Waislamu haki ya kuvaa vazi la Hijabu.

/3784788

Name:
Email:
* Comment: