IQNA

Akaunti ya Twitter ya Geert Wilders yasimamishwa kwa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu

17:02 - April 26, 2022
Habari ID: 3475170
TEHRAN (IQNA)-Twitter imeripotiwa 'kusimamisha kwa muda' akaunti ya kinara wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi Geert Wilders kwa kukiuka sheria za jukwaa kuhusu matamshi ya chuki baada ya kushambulia Uislamu tena.

Kulingana taarifa, Twitter imezuia kwa muda akaunti ya Wilders baada ya kuchapisha ujumbe alioulekeza kwa Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.

Katika tweet hiyo, mwenyekiti wa Chama cha Uhuru (PVV) alikashifu "vurugu za itikadi isiyo na ustahamilivu inayoitwa Uislamu".

Wilders pia alidai kuwa raia wa Pakistani ambao wamemtumia vitisho vya kifo "waliongozwa na nabii wa uwongo ..."

Wilders aliviambia vyombo vya habari vya Uholanzi kuwa amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na kukataa kuondoa machapisho kwenye akaunti yake. Wasifu wake kwenye Twitter hapo awali ulizuiwa mnamo 2019 baada ya kushutumiwa kwa kupanda chuki mtandaoni.

Kiongozi huyo wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia -- ambaye anaishi chini ya ulinzi -- anasema mara kwa mara amekuwa akipokea vitisho tangu alipotoa wito wa kupigwa marufuku Uislamu nchini Uholanzi na kufungwa kwa misikiti.

Mnamo 2020, mahakama ya rufaa ya Uholanzi iliidhinisha hukumu dhidi yake kwa kuwatusi raia wa Morocco katika maoni aliyotoa mwaka wa 2014, ingawa aliondolewa hatia ya kuchochea ubaguzi.

Waendesha mashtaka wa Uturuki pia wamemchunguza Wilders kutokana na ujumbe wa "kutusi" kuhusu Rais Recep Tayyip Erdoğan.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha PVV kwa sasa ndicho chama cha tatu kwa ukubwa nchini humo baada ya kushinda viti 17 katika uchaguzi mkuu uliopita wa Uholanzi mwaka 2021.

3478655

captcha