IQNA

Khatibu wa Sala ya Idul Adha Tehran

Watawala wa Saudia wafikishwe katika mahakama ya Kiislamu

22:14 - September 12, 2016
Habari ID: 3470560
Khatibu wa Sala ya Idul Adha Tehran amesema watenda jinai katika ukoo wa Aal Saud wanapaswa kufikishwa mbele ya mahakama ya Kiislamu na kuadhibiwa kutokana na maafa ya Mina katika ibada ya Hija mwaka jana.

Akihutubu katika Sala ya Idul Adha katika Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Ahmad Khatami amekosoa nchi za Kiislamu kwa kimya chao kufuatia jinai ya mwaka jana huko Mina na kusema, watenda jinai katika ukoo wa Aal Saud wanapaswa kufikishwa mbele ya mahakama ya Kiislamu na kuadhibiwa kwani hakuna yeyote aliye na shaka kuwa, katika maafa ya Mina mwaka jana, si tu kuwa watawala wa Saudia ni watuhumiwa bali pia ni watenda jinai na wahusika wa maafa hayo.

Aidha amesema maafa ya Mina mwaka jana ni thibitisho kuwa utawala wa ukoo wa Aal Saud haustahiki kusimamia Maeneo Mawili Matakatifu ya Waislamu.

Ayatullah Ahmad Khatami amesema kutokana na kutostahiki Aal Saud kusimamia Maeneo Mawili Matakatifu ya Kiislamu (Haramein Sharifein), kunapaswa kuundwa jopo la wasomi na viongozi wa nchi za Kiislamu kusimamia maeneo hayo au kwa uchache kusimamia Ibada ya Hija.

Ayatullah Khatami ameashiria kuhusu Mamufti wanaouza dini kwa ajili ya dunia huko Saudia na kuwataja kuwa watenda jinai sawa na ukoo wa Aal Saud.

Amesema mamufti ambao mafundisho yao ndiyo chanzo cha jinai za Wakufurishaji sasa wanajaribu kutetea jinai za ukoo wa Aal Saud.

Ayatullah Khatami amesema mashirika ya kimataifa nayo yanakabiliwa na mtihani mkubwa kwani baada ya kupoteza maisha Waislamu zaidi ya 7,000 katika maafa ya Mina hakuna tasisi yoyote ya kimataifa iliyotoa tamko kuhusu maafa hayo.

Khatibu wa Sala ya Idul Adha mjini Tehran amesema Iran imejitahidi kuhakikisha kunaundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu maafa ya Mina na kuongeza kuwa: "Usimamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu maudhui ya maafa ya Mina ni usimamizi unaopaswa kupongezwa na ni nembo ya namna Kiongozi anavyotetea haki za taifa lake."

Ayatullah Khatami pia ameashiria kufanyika kwa ufanisi mkubwa Dua ya Siku ya Arafa Jumapili na kusema: "Leo Umma wa Kiislamu unakabiliana na adui ambaye hataki Uislamu, wala hataki Waislamu wa Madhehebu ya Shia na Sunni na hivyo Waislamu wote wanapaswa kuungana kukabiliana na adui wao wa pamoja."

3529696

captcha